Thursday, 31 May 2018

Kauli ya Kinana kwa wanaccm


Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Ndg. Abdulrahman Kinana amewataka viongozi wa CCM kiujumla kumpa ushirikiano Katibu Mkuu mpya ambaye ni Dkt. Bashiru Ally kama walivyo kuwa wanampa yeye kipindi alipokuwa kwenye nafasi hiyo.

Kinana ametoa kauli hiyo leo Mei 31, 2018 nje ya Ofisi ya CCM iliyopo Lumumba Jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza makabidhiano ya ofisi na kiongozi huyo mpya ndani ya chama hicho.

"Nimekuja ofisini hapa na mwenzangu Katibu Mkuu CCM kufanya mambo matatu. La kwanza likiwa ni kumpongeza kwa kuteuliwa na Mwenyekiti na kuchaguliwa na Halmashauri Kuu Taifa la pili ni kumkabidhi ofisi na nimeshamkabidhi pamoja na makabrasha yanayohusika kwenye ofisi na la tatu nilikuwa na kazi ya kumtambulisha kwa watendaji ili aone kazi jinsi zilivyokuwa zikifanyika katika chama chetu na kuwaomba watendaji wampe ushirikiano kama walivyofanya kwangu", amesema Kinana.

Ndg. Kinana ameng'atuka kwenye nafasi hiyo siku za hivi karibuni huku akidai kilichopelekea kuchukua maamuzi hayo ni kutokana na umri wake kuwa mkubwa hivyo anahitaji kupumzika katika nafasi hiyo na kuwa mwanachama wa kawaida.

No comments:

Post a comment