Saturday, 14 April 2018

WANANCHI WAKINUKISHA OFISI YA SERIKALI


WANANCHI waishio Mwananyamala Kata ya Mbuyuni jijini Dar, hivi karibuni walikinukisha katika ofisi za serikali ya mtaa wao kufuatia madai ya ufisadi wa pesa walizokuwa wakichangishwa kwa ajili ya kubebewa takataka zao.

Tukio hilo lilijiri hivi karibuni ambapo umati mkubwa wa watu, wengine wakiwa na bodaboda walizingira ofisi hiyo wakipinga ukusanywaji wa fedha za takataka ambazo wanadai ni nyingi na wengine wanadai wanaonewa kwani wanatozwa hela pasipo kuwa na taka.

Wakifunguka kwa nyakati tofauti mbele ya Risasi Jumamosi, wananchi hao walisema kuwa wamechoshwa na mwenyekiti wao ambaye amekuwa akiwatoza fedha za takataka shilingi 3,000 kwa wiki ambazo kwanza ni nyingi lakini pia wanatoa wakati mwingine wakiwa hawana takataka.

“Tumekuja hapa ili kieleweke maana fedha ni ngumu sana, mtu huwezi kutoa fedha wakati huna taka, hivi inawezekana vipi?” alidai mmoja wa wananchi hao ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Hidaya.

Baada ya kuongea na wananchi wengi waliokuwa eneo hilo, Risasi Jumamosi liliongea na mwenyekiti wa mtaa huo, Uweso Nyange ambaye alifunguka na kusema kuwa, waliitisha kikao Machi 13, mwaka huu na wananchi walifika wengi na kukubaliana juu ya gharama za kubebea takataka.

“Kulikuwa na mkandarasi ambaye alikuwa akikusanya takataka na ikapangwa hela ya kila taka ambapo kila mwananchi alitakiwa atoe shilingi elfu moja kwa taka za kawaida lakini kiroba cha taka chenye uzito wa kilo 25 ni shilingi 2,000.

“Wananchi walikataa aina hiyo ya ukusanyaji taka, ikabidi tukubaliane kwa kupiga kura ambapo wengi walikubali kila nyumba itatoa shilingi 3,000 kila wiki na kama kutakuwa na wapangaji hela hiyo wataichangia,” alisema mwenyekiti huyo.

Aidha mwenyekiti huyo alisema kuwa, makubaliano hayo waliyafanya wote na wakakubaliana kila nyumba kutoa hela hiyo ambapo kama kutakuwa na nyumba hawajatoa, watalazimika kulipa tu hata kama nyumba hiyo haina taka kwani wanajua watu wanatupa taka dampo zisizo rasmi, kitu ambacho siyo sawa.

Baada ya kuongea na mwenyekiti huyo, gazeti hili lilimsaka mkandarasi aliyepewa tenda katika mtaa huo aitwaye Suleiman Ally ambaye alisema:

“Tunapata changamoto kubwa katika ukusanyaji wa pesa pamoja na takataka kwa kuwa mtaa una nyumba 930 lakini katika hizo nyumba 185 hawatoi pesa hiyo, hivyo kusababisha sisi kushindwa kuwalipa wafanyakazi.”

Hata hivyo, ilibainika kuwa, watu waliozua timbwili kwenye ofisi hiyo ya serikali ilitokana na baadhi yao kuwa na utaratibu mbaya wa kwenda kutupa taka kiholela na wanapofuatwa ili watoe taka zao, wanadai hawana na wakilazimishwa hapo ndipo tatizo linapoibuka.

No comments:

Post a comment