Monday, 16 April 2018

TRA Yasajili Wafanyabiashara Wapya 600 Mkoani Geita

Na Veronica Kazimoto,Geita,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesajili jumla ya wafanyabiashara wapya 600 katika kampeni maalum ya utoaji huduma na elimu kwa mlipakodi iliyofanyika mkoani Geita ikiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kodi pamoja na kusikiliza malalamiko, changamoto na maoni kutoka kwa wafanyabiashara hao.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa kampeni hiyo mwishoni mwa wiki, Menenja wa TRA mkoani hapa James Jilala ameishukuru Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa kufika mkoani Geita hususani katika maeneo ambayo hakuna ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na kufanikiwa kusajili wafanyabiashara wengi ndani ya wiki moja.

"Nianze kwa kuishukuru Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa hatua ambayo mmeifanya ya kufika katika Mkoa wetu wa Geita hasa maeneo ambayo hatuna ofisi ya TRA na  kufanikiwa kusajili wafanyabiashara wengi kwa muda mfupi kitu ambacho kimekuwa historia kwetu," alisema Jilala.

Jilala alisema kuwa, baadhi ya wafanyabiashara walishindwa kusajiliwa na kupatiwa  Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa wakati, kwasababu walitakiwa kusafiri zaidi ya kilomita 100 kwenda Geita mjini kwa ajili ya kupata huduma hiyo. Hivyo, zoezi hili limewarahisishia wafayabiashara kusajiliwa na kupatiwa TIN.

Naye Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu  Gabriel Mwangosi alisema kuwa , pamoja na usajili wa wafanyabiashara hao, shughuli mbalimbali zimefanyika katika kampeni hiyo ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali ya kodi kupitia semina na kuwatembelea katika sehemu zao za biashara.

"Katika zoezi hili tumefanya shughuli nyingi sana ikiwa ni pamoja na kuwatembelea wafanyabiashara mahali wanapofanyia biashara zao, tumesajili wafanyabiashara wapya na tumetoa semina mbalimbali  ambazo tunaamini kabisa  zitakuwa zimebadilisha mtizamo, utendaji na mwenendo mzima wa ulipaji kodi katika Mkoa huu wa Geita," alieleza Mwangosi.

Kampeni ya huduma na elimu kwa mlipakodi ni moja ya mikakati ambayo Mamlaka ya Mapato Tanzania imejiwekea katika kuhakikisha kuwa inasajili wafanyabiashara 1,000,000 katika mwaka huu wa Fedha wa 2017/18. 

Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: