Tuesday, 1 May 2018

MWIGULU AIFANANISHA SIMBA NA WATU WALIOKOSA KULA UBWABWA KWA MUDA MREFU


Na George Mganga

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Lameck Nchemba, ameifananisha Simba sawa na watu ambao hawajala ubwabwa kwa muda mrefu kutokana na namna wanavyoshangilia matokeo ya mchezo wa jana dhidi ya Yanga.

Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam likifungwa na Erasto Nyoni kwenye dakika ya 37.

Akizungumza na Radio EFM kupitia E Sports, Nchemba amesema kuwa Simba wanazungumza hivi sasa kutokana na mazingira ambayo yanaonesha kuwa wanaweza kuutwaa ubingwa wa ligi msimu huu baada ya kuukosa kwa takribani misimu minne.

Nchemba amewachukulia Simba kama watu ambao hawajala ubwabwa siku nyingi, kwa maana hiyo jana wamekula na kuanza kupiga kelele baada ya kuukosa kinywani kwa muda mrefu.

Kauli hiyo pia imekuja baada ya Spika wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai, kumtaja Nchemba kuwa amechelewa kuwasili Bungeni leo asubuhi sababu ya maumivu ya kufungwa na watani zake wa jadi Simba.

Ndugai alisema kuwa kuna baadhi ya Wabunge leo wamechelewa kuamka, akieleza kuwa bado wamelala kufuatia kipigo walichokipata Yanga kutoka kwa Simba, huku Nchemba akiwa ni mmojawapo.

No comments:

Post a Comment