MRITHI WA TUNDU LISSU KUJULIKANA KESHO - MSUMBA NEWS BLOG

Friday, 13 April 2018

MRITHI WA TUNDU LISSU KUJULIKANA KESHO


Utawala wa Tundu Lissu ndani ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) unafikia kikomo saa 24 zijazo wakati wanachama watakapomchagua mrithi wake.


TLS hufanya uchaguzi kila mwaka kupata viongozi ambao ni rais, makamu wa rais, mhazini na wajumbe wa baraza la uongozi.


Tayari mawakili wameanza kuwasili jijini Arusha kwa ajili ya mkutano mkuu wa uchaguzi na semina zitakazofanyika kuanzia leo.


Ni mkutano wa uchaguzi ambao Lissu hatakuwapo kwa kuwa yupo nchini Ubelgiji akitibiwa majeraha aliyoyapata Septemba 7 mwaka jana baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa ndani ya gari nje makazi yake mjini Dodoma.


Baada ya shambulio hilo, Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na siku hiyohiyo, alisafirishwa kwenda Hospitali ya Nairobi, Kenya kwa matibabu na Januari 6 alihamishiwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi.


Lissu anaondoka madarakani akiwa amekitumikia chama hicho kwa miezi sita tu kutokana na tukio hilo la kushambuliwa.


Wanasheria wanne wamejitokeza kumrithi ambao ni Fatma Karume, Godwin Mwalongo, Godfrey Wasonga na Godwin Ngwilimi ambaye sasa ni makamu wa rais.


Nafasi ya makamu wa rais inawaniwa na mgombea mmoja, Rugemeleza Nshala kama ilivyo ya uhazini inayowaniwa na Nicholas Duhia.


Wanaowania ujumbe wa baraza la uongozi ni Hussein Mtembwa, Stephen Axwesso, Aisha Sinda, Jeremia Mtobesya, Lambaji Madai, Goodluck Walter, Magdalena Sylister, Jebra Kambole na Frank Chundu.


Pilikapilika za mawakili hao jijini hapa zimeanza kuonekana idadi kubwa wameshawasili kuhudhuria mkutano huo pamoja na semina za kuwajengea uwezo.


Ofisa programu na maadili wa chama hicho, Anastazia Muro alisema leo kutakuwa na makongamano kwa ajili ya wanasheria wapya, wanasheria wanawake na kampuni katika maeneo tofauti jijini hapa.


Alisema mada zitakazowasilishwa zinalenga kuwajengea weledi katika kazi na miongoni mwa mada hizo zinahusu kodi, msaada wa kisheria na sheria ya utakatishaji wa fedha.


“Mkutano huu utahudhuriwa pia na wageni kutoka vyama vya wanasheria kutoka nchi mbalimbali zikiwamo za Afrika Mashariki na unatarajiwa kufunguliwa na Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambali,” alisema Muro.


Mmoja wa wagombea, Magdalena alisema wanataka rais atakayechaguliwa awe mtetezi wa masilahi ya mawakili wanaochipukia dhidi ya changamoto zinazowakabili katika kazi zao.


“Kazi zetu ni ngumu na tunapitia changamoto nyingi katika kuhakikisha wananchi tunaowawakilisha wanapata haki kwa wakati. Hivyo, tunataka kiongozi atakayekuja awe msikivu na kuwalinda mawakili,” alisema Magdalena


Alisema idadi kubwa ya mawakili walioanza kazi miaka ya karibuni wangependa kuona mzigo wa ada unapunguzwa kama alivyofanya Lissu na kutaka uwazi wa mapato na matumizi ya fedha za chama uongezwe.


Mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Arusha, Elibariki Maeda alisema wakiwa mawakili wenyeji, watashirikiana na wenzao kufanikisha mkutano huo ambao unalenga kubadilishana uzoefu na kujifunza mambo mapya.
Na Filbert Rweyemamu, Mwananchi
Comments


EmoticonEmoticon

Notification
This is just an example, you can fill it later with your own note.
Done