Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima (CCM) leo amehoji uhalali wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuagiza wanawake waliotelekezwa na waume zao wafike ofisini kwake na wapate msaada wa kisheria.

Pia ametaka baada ya akinamama kusaidiwa katika hilo, waitwe na akina baba waliotelekezwa na wake zao na kuachiwa watoto.

Sima alikuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Rais (Tamisemi) na ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2018/2019 mjini Dodoma leo Aprili 12.

“Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ametoa tamko na amefanikiwa akinamama zaidi ya 2000 wamefika pale, lakini nataka nifike mahali nishauri, Makonda amefanikiwa kwa sababu ameonyesha kuna mifumo ya serikali imeshindwa kufanya kazi yake, kwa mfano ustawi wa jamii, mifumo hii imeanguka,” amesema.

Hata hivyo, Sima amehoji Makonda anapata wapi mamlaka ya kisheria ya kuamua kuwaita akinamama hao?

Amesema kama ni jambo jema basi na wakuu wa mikoa wengine wanatakiwa wapate mamlaka ya kufanya kile anachokifanya Makonda.

“Ndugu zangu leo Makonda anatoa bima za afya, ni jambo jema sana, lakini kuna watoto yatima, hawana baba wala mama, nani atawapa bima za afya,” amesema.

Amesema anachotakiwa kufanya Makonda ni kuwasikiliza na kisha kuwarudisha katika mifumo rasmi iliyowekwa na Serikali.

“Naiomba Serikali kwenye eneo hili iwe makini sana, hasa wasaidizi wa Rais watambue kuwa wanatakiwa warudi kwenye mifumo rasmi,” amesema.

Sima ameomba kuwa baada ya jambo hili alilolifanya Makonda kwa akina mama wanaume waliotelekezwa nao waitwe na wasikilizwe  ili kuwe na usawa
Share To:

msumbanews

Post A Comment: