Tuesday, 17 April 2018

MAMA ALIA: DC WA JPM KANIZALISHA, KANITELEKEZA


WAKATI kizaazaa cha wanawake waliotelekezewa watoto na wanaume waliozaa nao kikiendelea kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es SalaamPaul Makonda, mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Magreth Wisaka ameibuka na kudai kutelekezewa mtoto na Mkuu wa Wilaya (DC) kutoka wilaya moja iliyopo mkoani Kigoma baada ya kumtaka aitoe mimba hiyo naye kukataa.

NI IJUMAA ILIYOPITA
Mwanamke huyo alikutana na mwanahabari wetu Ijumaa iliyopita kwenye ofisi za Makonda zilizopo Ilala-Boma jijini Dar alipokwenda kumlalamikia mteule huyo wa Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’.

ADAI KUHANGAIKA SANA
Mbele ya kinasa sauti cha Ijumaa Wikienda, mwanamke huyo alillia kuwa, ameshahangaika sana na DC huyo kumtaka wamlee mtoto wao huyo, lakini amekuwa akimpiga chenga.

ALIMUIBUKIA MWAKA JANA
Alisema kuwa, mwaka jana alimfuata DC huyo mkoani Kigoma anakofanyia kazi, lakini hata hivyo, maelewano hayakuwa mazuri na kuambulia kupewa shilingi laki tatu.
“Tangu aliponipa hiyo pesa, hataki tena mawasiliano na mimi nikimpigia simu ananiambia kuwa mkewe akigundua itakuwa balaa. Nikamwambia hata kama mkewe akigundua, mimi hainihusu. Ninachotaka ni matunzo ya mwanangu.

“Nilipoona hataki kunielewa, niliwatafuta ndugu zake ambapo nilifanikiwa kumpata kaka yake ambaye ni daktari ambapo mwanzoni alikuwa akinipa ushirikiano, lakini baada ya muda, naye akaanza kuninyima ushirikiano, nafikiri pengine ni baada ya kuwasiliana na ndugu yake.
“Ukweli kwa sasa ninaishi katika mazingira magumu sana na huyu mwanangu kwa maana mimi mwenyewe ninamlea kwa kazi ya kuuza maji na juisi pale Tabata jirani na ninapoishi, hivyo sina kipato kikubwa cha kuweza kumtunza mtoto.

“Nilishawahi kumlalamikia kwenye ofisi za Ustawi wa Jamii ambapo aliitwa na ulifikia muda tukaambiwa tukapime vinasaba (DNA), lakini nilipofika ofisi za Mkemia Mkuu, nikajikuta niko peke yangu, yeye hakutokea.
“Hivyo baada ya kulisikia zoezi hili hapa kwa Mkuu wa Mkoa nikaona kama Mungu amesikia kilio changu pamoja na wenzangu kama mimi,” alimaliza kusema Magreth kwa uchungu.
Baada ya kuzungumza na mwanamke huyo mwandishi wetu alimtafuta kwa simu DC huyo ambapo mambo yalikuwa moto;

Ijumaa Wikienda: Halooo… Halooo mheshimiwa DC (huku akimtaja jina).
DC: Naam ninakusikia.
Ijumaa Wikienda: Unamfahamu Magreth Wisaka?
DC: Mmm…Eee…we’ ongea tu.
Ijumaa Wikienda: Nakuuliza unamfahamu huyo mwanamke niliyekutajia?
DC: We ongea tu shida yako mi’ nakusikia tu.
Ijumaa Wikienda: Huyo mwanamke anakulalamikia kuwa umezaa naye na umemtelekeza mtoto, hebu tueleze vizuri ukweli ukoje?
DC: Mimi hilo suala siwezi kulizungumzia na huyo mwanamke wala simjui kwanza nilifikiri nimepigiwa na watu wa Makonda kumbe mwandishi…mimi sina la kuzungumza.
(Alimaliza kusema na kukata simu).
Mwanamke huyo akielezea historia ya kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mheshimiwa huyo alisema alikutana naye kwenye Baa ya Mremi’s iliyopo Buguruni ambapo wote walikwenda kupata huduma.
Magreth alimalizia kwa kusema kuwa, atafuatilia haki ya mwanaye hadi ajue mwisho wake na anachotaka kabla ya yote ni kipimo cha DNA.a
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: