Na Baraka Mbolembole
KLABU ya ZESCO United ya Zambia imetangaza kuingia mkataba na kocha wao wa zamani, George Lwandamina na kuzua hali ya sintofahamu klabuni Yanga SC.
Lwandamina alijiunga na Yanga, Novemba 2016 akichukua nafasi ya Hans van der Pluijm, na Mzambia huyo akafanikiwa kushinda ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara msimu uliopita-ikiwa ni taji la tatu mfululizo kwa mabingwa hao mara 27 wa kihistoria.
Kinachomwondoa Yanga
Uongozi wa Yanga chini ya kaimu mwenyekiti wa klabu, Clement Sanga kamwe sitaacha kuulaumu. Tangu alipojiuzulu, Yusuph Manji mara baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, nilishauri haraka kwamba-Yanga kama klabu ya wanachama inapaswa kuitisha mkutano ambao pia ungeipeleka katika uchaguzi mdogo-kujaza nafasi iliyoachwa na Manji.
Manji licha ya kukabiliwa na matatizo binafsi tangu Februari, 2017 lakini bado aliendelea kuwa upande wa klabu hadi pale walipofanikiwa kumaliza msimu. Alifanya maumuzi sahihi katika wakati mwafaka kwani aliamini klabu itakuwa na muda mzuri wa kujaza nafasi yake kabla ya kuanza kwa msimu huu-2017/18.
Manji alijiuzulu mapema mwezi Mei, lakini Kamati ya utendaji ya klabu imeshindwa kuidhinisha-kukubali­ kujiuzulu kwake, na badala yake Sanga akapewa nafasi hiyo kwa kilichosemwa-kukaimu­ kwa muda.
‘Nilikataa‘ katakata Sanga kukaimu nafasi hiyo. Wala sikuwa na shaka, niliandika makala tatu au nne. Ya kwanza ni mara baada ya Manji kuandika barua ya kujiuzulu, nikaandika tena wakati wa usajili wa kiangazi, nikafanya tena hivyo mara baada ya ‘suluhu ya kichovu‘ dhidi ya Tanzania Prisons katika uwanja wa Azam Complex Chamanzi mwezi Oktoba.
Mara zote nilisema nafasi aliyojipa Sanga ni kubwa mno kwake na kama kweli ni mtu wa Yanga alipangwa kuitisha uchaguzi mdogo kwa maana Yanga ina watu wengine wenye uwezo kama/karibia ya zaidi ya Manji.
Licha ya Yanga kuingia mkataba wa zaidi ya bilioni moja kwa mwaka na SportPesa mwezi Juni, 2017 lakini ndani ya miezi mitatu tu tangu kujiuzulu kwa Manji (Mei hadi Agosti) ‘migomo baridi‘ ilianza, wachezaji wakigoma kufanya mazoezi kutokana na malikimbikizo ya mishahara, posho na wengine pesa za usajili.
Sanga tayari alikuwa na uzoefu kuhusu migomo hiyo ya wachezaji kwasababu alikaimu nafasi ya Manji tangu Februari, 2017 wakati mwenyekiti huyo wa zamani wa klabu alipokabiliwa na matatizo. Wakati Vicent Bossou alipogoma kuichezea timu hiyo mwezi Machi iligundulika klabu haikuwa imelipa mishahara ya wachezaji kati ya Disemba, 2016-Februari, 2017.
Ni Wakati wa mwanzo wa misukosuko ya Manji. Uzoefu huu ulinipa sababu za kuitaka kamati ya utendaji kuipeleka klabu katika uchaguzi mdogo wa kumchagua mwenyekiti mpya.
Lakini kama nilivyopata kuandika katikati ya mwaka uliopita kwamba-Sanga ni mtu anayependa kujikuza haraka kiuongozi licha ya kwamba bado hana uwezo mkubwa. Niliposema ‘anguko‘ la Yanga litaletwa na Sanga, wapo wengine wanachama wa klabu hiyo walisema ‘nisiwafuate-fuate‘.­
Uongozi wa Sanga umekuwa ukiwahadaa wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kwa kuficha baadhi ya mambo muhimu-kama madai ya mishahara ya wafanyakazi, wachezaji, benchi la ufundi. Kuna wachezaji wamekuwa wakigoma kucheza kwa kwa madai kama hayo lakini uongozi umekuwa ukidanganya kuwa ni majeruhi.
Lwandamina, nampongeza sana kwa busara zake, sijawahi kusikia akilalamika mahala kuhusu madai ya mishahara yake na posho lakini kocha huyo alikuwa akidai zaidi ya mshahara wa miezi mitatu hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu. Ameondoka Yanga kwa kile kinachosemwa kumalizika kwa mkataba wake lakini ili si jambo la kweli.
Lwandamina aliingia Yanga mwezi Novemba 2016 na ilitajwa amesaini mkataba wa miaka miwili kwa maana hiyo kwa namna yoyote ile kocha huyo alikuwa na mkataba lakini hali ya mambo imemshinda na kuamua kurejea ZESCO ambao wamefuzu hatua ya makundi ya Caf Champions League huku akiiacha Yanga mguu mmoja ndani kufuzu kwa hatua ya makundi ya Caf Confederation Cup msimu huu. Lwandamina ameondoka kwa sababu za kimaslahi, hili lifahamike wazi hata kama uongozi utatoka na kusema ‘alimaliza mkataba.’
Sanga nitaendelea kumlaumu kwa kila kitu kinachokwenda ‘mrama’ hivi sasa ndani ya Yanga kwa sababu amekuwa ‘akitumia mbinu chafu’ kupeleka mambo kuna baadhi ya marafiki zake katika media na hao kila mambo yanapokwenda hovyo wamekuwa ‘wakitumwa’ kuandika ‘bosi arejea Yanga’ ujinga mtupu.
Manji niliwaambia tamngu Disemba, 2016 kuwa anataka kuachana na Yamnga na baada ya misukosuko yake nikasisitiza ni ndoto kuamini kuwa Manji ataisaidia Yanga kiuchumi, ukweli anatamani kudai pesa anazoidai klabu hiyo lakini kwa uungwana, mapenzi yake kwa klabu, busara zake ameona hali halisi ilivyo.
Uongozi umekaa kimya kuhusu kuondoka kwa Lwandamina, jambo hili ni baya, linawachanganya wachezaji, wanachama na mashabiki kwa maana kocha mkuu ameondoka timu ikiwa katika vita ya ubingwa huku michezo nane ikiwa imesalia (kabla ya Yanga v Singida United) Jumatano hii. Yanga wana safari ya Ethiopia kurudiana na Wolaitta Dicha, lakini nani sasa anaweza kuwa mtu sahihi wa kuchukua nafasi ya Lwandamina mwezi mmoja kabla ya kumalizika kwa ligi, wiki mbili kabla ya kuwavaa Simba?
Kwa nini imefanywa siri mno kuhusu kuondoka kwa Lwandamina Yanga? Kwa nini uongozi umeshindwa kufanya jitihada haraka za kumsaka kocha mpya kama kweli ilifahamika April 6 ndiyo mwisho wa mkataba wa Lwandamina? Siamini kama mtu hasa wa Yanga kama Sanga anaweza ‘kuitumbukiza’ klabu yake shimoni.
Nina jiuliza maswali mengi mno kuhusu mwaka mmoja wa Sanga kama mwenyekiti wa kukaimu.
Lwandamina alisaini mkastaba wa muda gani Yanga wakati anajiunga Novemba 2016? Kila la heri kocha wewe mkimya, ambaye sijui ulikuwa na lengo gani Yanga, ila niliona kikosi bora cha wazawa chini yako ndani ya mwaka mmoja ujao. Kazi njema huko ZESCO, Yanga ni masikini tangu ilipoanzishwa, ni masikini wa fikra za kiongozi. Ndio maana sikukuelewa japo nilikuwa najenga imani yangu taratibu kwako.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: