Sunday, 1 April 2018

Jeneza la Maajabu laonekana Mbeya


NELSON Edson, mkazi wa Mtaa wa Nsalaga Kata ya Nsalaga jijini hapa amejikuta kwenye taharuki kubwa baada ya kuamka na kukuta jeneza tupu dogo nje ya mlango wa nyumba yake.

Tukio hilo lililoibua hekaheka mtaani hapo lilijiri asubuhi ya Machi 27, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Nsalaga, Paul Ngonde, alipokea taarifa kutoka kwa Edson na kuamua kwenda eneo la tukio ili kushuhudia.
Alisema kuwa, baada ya kuwashirikisha wazee wa mila juu ya jambo hilo, walilifungua jeneza hilo na kukuta likiwa tupu, lakini likiwa na sanda nyeupe iliyoviringishwa ndani yake.

“Nimeshangaa asubuhi kuamka na kukuta jeneza nje ya mlango wa nyumba yangu, sijaelewa ni nini madhumuni ya kuwekewa jeneza hilo,” alisema Edson huku akionesha kustaajabishwa na tukio hilo.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, mtaa huo umekuwa na matukio ya ajabuajabu yakiwemo ya kutupa watoto, lakini tukio hilo la jeneza limekuwa ni tukio la kwanza kutokea mtaani kwake.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, DCP Mohammed Mpinga alikiri kutokea kwa tukio na kwamba jeshi lake linafanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo huku akiwataka wanachi kutulia.
Stori: Ezekiel Kamanga, Mbeya
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: