Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, ameishauri serikali kufuatilia kwa makini kupaa kwa deni la matibabu ughaibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kuwasilisha bungeni mjini hapa ripoti yake ya ukaguzi ya mwaka 2016/17, Prof Assad alisema ukaguzi wake kuhusu gharama za matibabu ughaibuni ulibaini ongezeko kubwa la deni kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika hospitali za India.

Alisema deni hilo limepanda kutoka kiasi cha Sh. bilioni 28.6 kilichoripotiwa Juni 30, 2017 hadi Sh. bilioni Sh. 45.73 kufikia Desemba 31, 2017 licha ya serikali kuweka masharti kwa wananchi kwenda kutibiwa kwenye hospitali za nje ya nchi.

“Ongezeko hili ni asilimia 60.71 kwa kipindi kifupi, ni jambo linalohitaji serikali kulifuatilia kwa makini ili kupunguza mzigo wamadeni na kuhakikisha kuwa hospitali husika zinalipwa kwa wakati,” alisema.

Kuhusu Deni la Taifa, Prof. Assad alisema limeongezeka kwa Sh. trilioni 5.04 katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Juni 2016 hadi Juni 2017.

Alibainisha kuwa hadi kufikia Juni 30, 2017, deni hilo lilikuwa Sh. trilioni 46.08 likipanda kutoka Sh. trilioni 41.03 lilivyokuwa Juni2016, ikiwa ni ongezeko la Sh. trilioni 5.04 (asilimia 12).

Alisema kuwa kati yake, deni la ndani ni Sh. trilioni 13.33 na deni la nje ni Sh. trilioni 32.75.

Prof. Assad alisema kiasi cha Sh. trilioni 4.58 hakikujumuishwa katika Deni la Taifa kutokana na kutojumuishwa kwa madeni ya mifuko ya pensheni pamoja na dhamana ambazo masharti yake yalikiukwa.

CAG Assad alibainisha vigezo vitatu vinavyotumika kupima uhimilivu wa Deni la Taifa akibainisha kuwa uwezo wa nchi kulipa riba ya deni ulikuwa umefikia karibu mwisho, lakini mwaka huu wametumia kigezo cha GDP kulingana na deni hilo.

”Kwa kutizama kigezo hicho, tumesema ni himilivu, lakini kama nilivyosema siyo busara kutizama kipengele hicho na kusema tunaweza kukopa kwa sababu tulishawahi kukopa tukapunguziwa mkopo,” alisema.

”Kwa hiyo, mimi rai yangu ni lazima tuwe waangalifu katika ukopaji wetu. Deni la Taifa linapimwa kwa namna nyingi, na zipo namna tatu kubwa; ya kwanza ni ile ya kuangalia deni kulinganisha na Pato la Taifa, lakini pia ujue kwamba unachotakiwa kufanya ni kuangalia malipo ya mbele ulinganishe na thamani ya fedha ya sasa.

”IMF na Benki ya Dunia (WB) kazi yao ni hiyo kuangalia data (takwimu) za kila nchi. Njia ya pili ni kuangalia mapato ya nchi dhidi ya Deni la Taifa. Kwa mfano, tunakusanya kiasi gani cha kodi? Hili ni eneo ambalo ni ‘sensitive’ zaidi, ile ya mwanzo ni kiunzi cha chini sana ndo maana unaweza kukuta nchi ina asilimia 200 kwa sababu ni kiunzi cha chini sana.

”Njia ya tatu ni kuangalia Deni la Taifa dhidi ya ‘export’ kwa sababu sehemu kubwa ya Deni la Taifa utailipa kwa fedha za nje.”Alisema mwaka huu kwa kulinganisha Deni la Taifa na GDP, deni hilo linamilika, lakini lazima nchi ambayo iliwahi kupewa nafuu ya mkopo, isikimbilie kukopakopa.

”Hatuwezi kusema tutakopa tutakopa, tutakopa kwa tahadhari kubwa kwa sababu hatutaki kurudi miaka 20 iliyopita sehemu ambayo tunataka tupewe msamaha wa madeni,” alisema.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: