WATU wawili wamefariki dunia katika mlipuko wa moto uliotokea kwenye kituo bubu cha kuuza petroli wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.

Katika tukio hilo majeruhi mmoja, Pili Omari (19), amelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo, baada ya kupata majeraha ya moto sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, alisema tukio hilo lilitokea Machi 25 saa saba mchana katikaKitongoji cha Mgambo Kata ya Kwamagome  Wilaya ya Handeni.

Kwa mujibu wa Bukombe, waliofariki kwenye tukio hilo ni Hamis Mkuruto (45) ambaye ni mfanyabiashara wa mafuta hayo na Ally Haji maarufu kwa jina la ‘Tofiki’ (17) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi, Maingi Kwamagome.Kamanda Bukombe alisema chanzo ni sigara iliyokuwa ikivutwa na Hamisi wakati akipima petroli na kusababisha mlipuko mkubwa wa moto uliosababisha madhara hayo.

“Baada ya miili ya marehemu kufanyiwa uchunguzi na madaktari ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko,” alisema Kamanda Bukombe.

Hata hivyo, alisema hasara ya mali iliyotokana na ajali hiyo haijafahamika na hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Katika tukio lingine, lilitokea juzi asubuhi katika Kitongoji cha Chikago Kijiji cha Kwabojo Kata ya Mgambo wilayani Handeni, Yahaya Juma (65), ambaye ni mkulima aliuawa kwa kuchomwa kisu na mtu aliyetajwa kwa jina moja la Mang’ati.

Kamanda Bukombe alisema chanzo cha mauaji hayo ni marehemu kupishana kwa maneno na Mang’ati aliyemtania binti wa kike wa Yahaya kuwa anataka kumuoa, jambo ambalo lilipingwa na mzazi huyo, hivyo kumchoma kisu sehemu ya bega la mkono wa kushoto.

Alisema marehemu alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa hospitali ya Wilaya kwa ajili ya matibabu,
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, baada ya taarifa za kifo hicho, wananchi wenye hasira walimvamia Mang’ati na kumshambulia hadi kupoteza maisha.

Bukombe alisema Jeshi la Polisi linaendelea na msako kuwakamata waliohusika na mauaji ya Mang’ati, na kukemea tabia za wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: