Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha amewataka watumishi wapya wa Wizara hiyo kuwa waadilifu katika utendaji kazi  pamoja na kutunza siri katika maeneo wanayofanyia kazi.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa rai hiyo mjini Dodoma wakatiwa akifunga  mafunzo kwa waajiriwa wapya wa Wizara hiyo mafunzo ambayo yamelenga kuwakumbusha, taratibu, sheria na miongozo ya kazi inayotakiwa  katika utumishi  wa Umma.


Naibu Waziri huyo amesema  anaamini mafunzo yaliyotolewa yatawawezesha  kuwa watumishi bora wa umma  ambao wanafahamu vema mikapa ya kazi, taratibu za kiutumishi, lakini pia haki na wajibu katika utendaji kazi.

Pamoja na mambo mengine Naibu Waziri Ole Nasha amemuagiza Mkurugenzi wa Utawala na  Rasilimali watu wa Wizara hiyo Moshi  Kabengwe kuandaa utaratibu wa mafunzo kwa watumishi wengine wa Wizara hiyo  ili kuwakumbushia taratibu, kanuni na miongozo  ili kuepuka ukiukaji wa maadili na pia Kuleta Chachu ya mabadiliko katika utendaji kazi miongoni mwa watumishi.

Nae mmoja wa watumishi aliyeshiriki mafunzo hayo Lazaro Julius  kutoka Ofisi ya Kamishna  wa Elimu wa Wizara hiyo amesema  mafunzo hayo ni muongozo thabiti katika kutekeleza majukumu ya kazi za kila siku katika utumishi wa Umma,ambapo ameahidi kuzingatia na kutekeleza yote aliyoelekezwa.

Mafunzo  kwa waajiriwa wapya wa Wizara hiyo yamefanyika kwa siku nne  kuanzia Machi 6, 2018 na yameshirikisha waajiriwa wapya kutoka Wizara ya Elimu Makao Makuu, na Taasisi zilizochini ya Wizara hiyo.

Imetolewa na;

Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia

9/3/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: