BENKI ya Exim, imeahidi kutoa vitanda na magodoro 500 katika hospitali za serikali katika mikoa 13 nchini, kama sehemu ya kampeni yake yenye lengo la kusherehekea miaka 20 ya kutumikia jamii.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vitanda na magodoro 40 kwa Hospitali ya Rufani ya Bombo mkoani Tanga jana, Mkuu wa Idara ya Masoko wa benki hiyo,  Stanley Kafu, alisema wanaamini katika kuhudumia jamii.

"Katika kipindi cha miaka 20, benki imetambua umuhimu wa jumuiya zinazozunguka eneo la biashara yetu na ndio maana shughuli za kijamii ni muhimu," alisema Kafu na kueleza zaidi:

"Tunaamini kwamba tuna sehemu kubwa katika kufanya mabadiliko mazuri katika sekta mbalimbali katika jamii zetu.

"Ni kwa hili benki iliamua kusherehekea miaka 20 kwa kusaidia jamii kwa njia ya kampeni inayoitwa, 'Miaka 20 ya Kujali Jamii' kuonyesha jinsi tunavyowashukuru.

"Benki ya Exim itatoa vitanda na magodoro ya hospitali kwa hospitali nchini kila mwezi kwamwaka mzima."

Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga ni ya saba kupokea mchango huo, baada ya Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mbeya, Mount Meru (Arusha), Dodoma, Ligula (Mtwara), Mnazi Mmoja (Zanzibar) na Temeke ya jijini Dar es Salaam.

Naye Ofisa wa Matibabu wa hospitali hiyo, Dk. Clemence Marcelli, mbali na kuipongeza benki hiyo alisema kwa kiasi kikubwa msaada huo umepunguza uhaba wa vitanda uliokuwa ukikabili.

"Upungufu wa vitanda katika hospitali ni changamoto kubwa," alisema Dk. Marcelli hivyo "msaada huu kutoka benki ya Exim wa hivi vitanda 40 na magodoro utasaidia sana katika kupunguza changamoto hii."

Hospitali nyingine zinazotarajiwa kunufaika ni za mikoa ya Mwanza, Morogoro, Tanga, Dodoma, Kigoma, Kilimanjaro, Shinyanga, Mtwara, Dar es Salaam, Pemba na Unguja.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: