Wednesday, 14 March 2018

Askari Magereza waendelea kusota rumande


ASKARI Magereza 11 Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wanaodaiwa kumuua mwanakijiji, Aloys Makalla, wanaendelea kusota mahabusu, baada ya kesi yao kuahirishwa.

Kesi hiyo iliahirishwa tena jana kwa mara ya nne na Mahakama ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Askari hao wanaotuhumiwa kumuua Makalla, mkazi wa Kijiji cha Kerenge, Kata ya Kerenge, Wilaya ya Korogwe.Hakimu  Mfawidhi wa Mahakama hiyo,  Albert Nyang’ali, ambaye alisoma shtaka hilo la mauaji kama mlinzi wa  amani, alisema sababu ya kuendelea kutajwa shauri hilo bila kupangiwa kusikilizwa ni kutokana na baadhi ya vipengele kufanyiwa marekebisho.

Nyang’ali aliwataja askari hao ambao wapo mahabusu ya Gereza la Wilaya ya Korogwe ni P. 5377 Inspekta Makere, A. 4921 RSM (Mkuu wa Nidhamu) Mokiwa Shadrack Lugendo, A. 7367 Sajenti Mussa Mdoe Seif, B. 5919 Koplo Lazaro Stephen Nyato, B. 5486, Koplo Ramadhan Yusuph, B. 7087 WDR Robert Alfred, B. 7980 Fidirishi Cosmas Joseph, B. 7248 WDR Alphonce Revocatus, B. 8911 WDR Mbesha Naftari,  B. 9747 WDR Michael Elias Michael na B. 8533 WDR Hamis Halfa Msola.Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa watuhumiwa wote kwa pamoja Januari 22, 2018 katika Kijiji cha Kerenge wilayani Korogwe walimuua Aloyce Makalla maarufu kama Mapi.Katika kesi hiyo namba 2 P I ya mwaka 2018, watuhumiwa wote walikana shtaka, lakini hawakutakiwa kujibu chochote kwa vile mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.Shauri hilo limepangwa kutajwa tena Machi 26, mwaka huu. Hii ni mara ya nne kesi hiyo kutajwa huku, watuhumiwa wote wakirejeshwa rumande.

No comments:

Post a comment