Siku 100 bila Azory Gwanda 

Leo ni siku ya 100 tangu mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda alipotoweka katika mazingira ya kutatanisha.
Gwanda aliyekuwa akiishi na kufanya kazi wilayani Kibiti, Pwani alitoweka Novemba 21, 2017 na tangu wakati huo hajaonekana na hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusu mustakabali wake.
Mara ya mwisho, Azory alionekana akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe na kwa mujibu wa Anna Pinoni, ambaye ni mkewe, alichukuliwa na watu wasiojulikana alipokuwa katika eneo ambalo hupenda kukaa kwa maongezi na wenzake.
Baada ya kumchukua, walikwenda naye shambani alipokuwa mke wake huyo ambako alimuuliza mahali ulipokuwa ufunguo wa nyumba yao na baada ya kumwelekeza, Azory aliondoka huku akimwambia kuwa anakwenda kazini na angerudi jioni ya siku hiyo au siku iliyofuata ambayo ilikuwa ni Jumatano.
Mkewe aliporudi nyumbani alikuta dalili ya kupekuliwa kwani aliona vitu mbalimbali vikiwa vimerushwa shaghalabaghala ndani ya nyumba, “Sikuwa na shida, mpaka siku iliyofuata baada ya kuona simu zote za mume wangu hazipatikani. Alhamisi ya Novemba 23, nilikwenda kuripoti Kituo cha Polisi Kibiti ambako nao walisema hawajui alipo na wakaniomba niwape namba yake ili wajue alipo.”
Taarifa za kutoweka kwake ziliifika MCL ambayo ilifanya jitihada za kujua aliko pasi na mafanikio.
Desemba 7, mwaka jana kampuni hiyo iliitisha mkutano wa wafanyakazi uliohudhuriwa pia na waandishi wa habari kwenye ofisi zake Tabata, Relini jijini Dar es Salaam ambako mkurugenzi mtendaji wa MCL, Francis Nanai alisema baada ya kupata taarifa hizo, waliwasiliana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji ambaye alisema hakuwa na taarifa na kwamba watafuatilia na kutoa taarifa.
Pia MCL iliandika barua rasmi kwa waziri wa habari, mkuu wa Jeshi la Polisi, Spika wa Bunge, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Taasisi ya Misa Tan, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, licha ya juhudi zote hizo mpaka sasa bado haijajulikana waliomchukua ni kina nani, wametumwa na nani na wamefanya hivyo kwa malengo yapi.
Katika mkutano huo Nanai alitoa rai, “Kama ameshikiliwa kwa kosa lolote alilofanya, basi aliyemshikilia ampeleke kwenye vyombo vya kutoa haki ili haki itendeke. Tungependa kumpata Azory akiwa hai ili ashirikiane nasi katika kulijenga taifa letu.”
Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga aliyekuwepo kwenye mkutano huo alisema tukio hilo lina kila dalili ya uovu, kwani kama Azory angekuwa amefanya uhalifu angepelekwa kwenye vyombo vya sheria.
“Sisi kama tasnia ya vyombo vya habari tunadhani kuna nia ovu kukamatwa kwa Azory. Kwa sababu kama kuna jambo amefanya ilitakiwa atiwe hatiani halafu apelekwe mahakamani,” alisema Makunga na kuongeza kuwa kitendo hicho kinatishia uhuru wa habari na waandishi kufanya kazi zao hivyo akawataka wadau wa habari kuendelea kupiga kelele ili kuhakikisha Azory anarudi kwenye kazi yake.
Mjumbe wa TEF ambaye pia ni mhariri wa gazeti la Raia Mwema, Godfrey Dilunga alisema tukio hilo limeleta picha mbaya kwenye ulinzi wa vyombo vya habari na kuwataka waandishi wa habari kuungana.
“Nashauri waandishi tuwe pamoja, hatuna uhakika haya masuala yataishia wapi, kwa hiyo umoja ni suala muhimu sana. Kazi yetu inahitaji umoja na ushirikiano wa kati yetu na wananchi,” alisema Dilunga.
Tangu wakati huo, polisi imekuwa ikisema inaendelea na uchunguzi wa suala hilo na hivi karibuni wakati wa kumwapisha Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohamed Hassan Haji, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alisema wanaendelea kulifanyia kazi jalada la kupotea kwake. “Tunaendelea kukusanya taarifa na ushahidi kuhusiana na kutoweka kwa Gwanda, hivyo mwananchi mwenye taarifa asisite kutuletea, zitakuwa siri kati yetu na yeye na tutazifanyia kazi kuhakikisha mwandishi huyo anapatikana,” alisema Sirro.
Februari 13 mwaka huu, Anna, ambaye ni mke wa Azory alijifungua mtoto wa kike anayeitwa Gladness kwani wakati mumewe anatoweka alimuacha akiwa na ujauzito wa miezi sita.

Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: