Saturday, 24 February 2018

Serikali yaitaka mgodi kuwalipa fidia wananchi

Serikali imetoa siku mbili kwa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kukamilisha mchakato wa ulipaji fidia wa nyumba zaidi ya 80 za wananchi zilizopata nyufa kutokana na milipuko ya shughuli za ulipuaji miamba.

Wananchi wa Nyamalembo wanaoishi karibu na mgodi huo wamekuwa na malalamiko ya zaidi ya miaka mitano wakilalamikia nyumba zao kupata nyufa zinazosababishwa na milipuko, huku Serikali kupitia Wizara ya Madini ikiagiza mara kwa mara mgodi kulipa fidia bila utekelezaji.

Akizungumza jana Februari 23,2018 na wananchi wa Nyamalembo na Katoma wanaozunguka mgodi wa GGM ambao wamekuwa na malalamiko ya miaka mingi, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema madai ya wananchi sasa yamefika mwisho.

Amesema migogoro mingi katika sekta ya madini inawezekana inasababishwa na upungufu wa sheria za madini na kusema pamoja na sheria na kanuni mpya kutungwa, bado zipo sheria zinasababisha matatizo kwa wananchi.

“Kama sheria inaonekana ni kikwazo au inasababisha matatizo kwa jamii hatutaona tabu kurudi nyuma na kuirudisha bungeni kufanyiwa marekebisho,” amesema.

“Nia yetu sio kumkandamiza mwananchi, bali ni kutaka

mwananchi aone maendeleo ya kuwa na mwekezaji katika maeneo yenu na hatuoni sababu ya mwekezaji kuwa kero kwa wananchi.”

Amesema kama zipo sheria na kanuni zinazombana mwekezaji kutoa haki kwa mwananchi, Serikali ipo tayari kuzirekebisha na kuwataka wawekezaji kutotumia udhaifu wa kisheria kumkandamiza mwananchi.

Katika hatua nyingine, Nyongo ameutaka mgodi huo kuwalipa fidia wananchi wa Mtaa wa Katoma wanaoishi ndani ya leseni za mgodi, na kama hawapo tayari kuwalipa wawaachwe waendeleze shughuli zao na kuitaka halmashauri kuwapa wananchi hati za ardhi ili waweze kupatiwa huduma ya maji na umeme.

Makamu wa Rais wa Anglo Gold Ashanti, Simon Shayo amesema masuala mengi yanayolalamikiwa yapo kisheria na kuomba yatizamwe kwa mujibu wa sheria ili haki itendeke kwa pande zote mbili.

No comments:

Post a comment