Tuesday, 20 February 2018

Naibu Waziri wa Maji atoa agizo kwa Dawasa na Dawasco


Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso ameziagiza DAWASA na DAWASCO kuhakikisha zinafikisha huduma ya maji kwenye maeneo yaliyo pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam, ambapo kuna uhaba mkubwa wa maji pamoja na kuwa na wakazi wengi zaidi na si kujikita katikati ya jiji hilo tu.

Naibu Waziri Aweso ametoa agizo hilo akiwa katika ziara ya kikazi katika Wilaya ya Temeke kujionea uhalisia wa utekelezaji wa miradi ya maji, wilaya ambayo imekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na huduma hafifu ya majisafi  na salama.

Aweso amesema kuwa kuna haja ya DAWASA na DAWASCO kuimarisha huduma ya maji kwenye maeneo ya pembezoni mwa jiji kama Temeke, Kigamboni, Ukonga, Mbagala na Segerea ili kukidhi mahitaji makubwa ya maji kwa wakazi wengi wanaoishi maeneo hayo.

''Fanyeni utaratibu wa kukarabati miradi ya zamani kama hatua ya kwanza na ya haraka ya kuwapatia wananchi maji, wakati mkiendelea kutekeleza miradi mipya na mikubwa ambayo utekelezaji wake utachukua muda mrefu. Mmejikita sana katikati ya jiji, ambapo kwa sasa huduma hiyo imeimarika kwa kiasi kikubwa. Umefika wakati wa kuwekeza maeneo ya pembezoni kwa sasa, na wakazi hawa nao wafurahie huduma ya maji ya uhakika'', aliagiza Naibu Waziri Aweso.

Aidha, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji alitoa onyo kwa manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam kutowapa kazi wakandarasi wasio na uwezo. Pia, kuchukua hatua stahiki kwa wakandarasi wote wanaosuasua katika utekelezaji wa miradi, huku akiwahakikishia wakandarasi wote kulipwa fedha zao kwa wakati ili wasikwame katika utekelezaji wa miradi hiyo.

No comments:

Post a comment