Monday, 12 February 2018

Maafisa utumishi watakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo amewataka Maafisa Utumishi wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuongeza ari ya watumishi wa umma katika kutoa huduma zenye ubora kwa wananchi.

Akizungumza wakati akifungua Kikao Kazi cha Siku mbili kilichowahusisha Wakurugenzi wa Rasilimali watu wa Wizara zote, Idara zinazojitegemea na Maafisa Utumishi wa Halmashauri zote hapa nchini mapema leo mjini Dodoma Waziri Jafo amesema kuwa ni dhamira ya Serikali kuona changamoto za Watumishi wa Umma zinatatuliwa kwa wakati.
“Maafisa Utumishi mnalo jukumu kubwa lakuwasaidia watumishi katika maeneo yao kwa kufanya kazi zenu kwa kuzingatia weledi, kuepuka rushwa, vitendo vya upendeleo na mambo yote yanayoweza kuchafua taswira ya Serikali kupitia huduma mnazotoa” Alisisitiza Mhe. Jafo
Akifafanua zaidi Waziri Mhe. Jafo amesema kuwa wajibu wa Maafisa Utumishi ni kuwa Kiungo kati ya Wakurugenzi na watendaji wa Taasisi hali itakayosaidia kupunguza au kuondoa malalamiko yanayofikishwa Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Aliongeza kuwa Maafisa Utumishi wanajukumu kubwa katika kuhakikisha watumishi wanapandishwa madaraja kwa wakati, wanathibitishwa kazini kwa wakati ili kuwaongezea morali kwa watumishi hali itakayoongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Pia aliwaasa Maafisa Utumishi kuhakikisha kuwa Wanatunza taarifa zote za Watumishi kwa kuzingatia sheria , Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma ili kulinda maslahi mapana ya nchi.
Kwa upande Wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Musa Iyombe amewataka Maafisa Utumishi wote kufanya kazi kwa kuzingatia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kuleta mabadiliko kwa wananchi kwa kuwapa huduma bora.
Aidha, Mhandisi Iyombe aliwaasa kuacha kufanya kazi kwa mazoea hali inayopelekea kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa watumishi na hivyo kuzorotesha kasi yakuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Bw. Mathias Kabunduguru akizungumza katika Kikao Kazi hicho amesema kuwa baadhi ya masuala yanayoleta kero kwa watumishi wa Umma ni pamoja na Mamlaka za Ajira kukataa kuidhinisha au kupitisha barua za watumishi kuhama, hivyo aliwaasa Maafisa hao kutozuia maombi ya watumishi wanaoomba kuhama.
“Mamlaka husika inaweza kuweka maoni yakuomba mbadala wa Mtumishi anayeondoka na sikuzuia barua yake yakuomba uhamisho kwa kuwa uhamisho wa watumishi unajengwa kwa Misingi ifuatayo, kwanza mtumishi anayohaki ya kufanya kazi popote,Uhamisho hujenga Afya ya Utumishi kwa ujumla na pia swala hilo husaidia Kujenga umoja wa Kitaifa.
Aliongeza kuwa Kikao Kazi hicho kitakuwa chachu ya kuimarisha Uadilifu,Uwajibikaji,Uwazi, na misingi mingine ya Utawala Bora.
”Pamoja na Kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa Vyeti vya Kidato cha nne, Sita, Ualimu na Vyuo Vikuu bado wapo waajiri aidha kwa makusudi au kwa bahati mbaya wameendelea kuwafumbia macho watu wenye vyeti bandia ambapo wiki iliyopita tulilazimika kuchukua hatua kali dhidi ya Maafisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kutokana na kuficha watu wenye vyeti Bandia,” Alisisitiza Bw. Kabunduguru.
Akizungumzia swala la kutambua mchango wa watumishi wanaofanya kazi kwa bidii Bw. Kabunduguru amesema linaongeza ari yao katika kutekeleza majukumu yao hivyo ni vyema utaratibu wa kuwatambua hata kwa kuwaandikia barua za kutambua mchango wao na pia kuwaadhibu watumishi wazembe wasiotekeleza majukumu yao.
Kikao Kazi hicho cha siku Siku mbili kilichowahusisha Wakurugenzi wa Rasilimali watu wa Wizara zote, Idara zinazojitegemea na Maafisa Utumishi wa Mikoa, Halmashauri zote hapa nchini kinafanyika mjini Dodoma kimeandaliwa kwa ushirkiano wa Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala bora na Ofisi ya Rais TAMISEMI kikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuimarisha utendaji na huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: