Friday, 16 February 2018

Haya ndio Wanayopaswa kufanya wapigakura Kinondoni, Siha


Kesho Jumamosi wananchi katika majimbo ya Kinondoni, Dar es Salaam; Siha mkoani Kilimanjaro na wenzao katika kata tisa nchini wanakwenda kupiga kura kuchagua wabunge na madiwani. Huu ni uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizokuwa wazi lakini uliobeba sura ya kitaifa kutokana na jinsi ulivyowakusanya vigogo wa vyama vya siasa kwenye kampeni na hivyo kusababisha ushindani mkali. Kata zinazoshiriki uchaguzi ni Isamilo (Nyamagana), Manzase (Chamwino), Madanga (Pangani), Mitunduruni (Singida), Kanyelele (Misungwi), Buhangaza (Muleba) pamoja na Donyomurwak, Gararagua na Kashashi wilayani Siha. Kata ya Kimagai (Mpwapwa) mgombea wa CCM alipita bila kupingwa.

Ili kufanikisha shughuli hiyo wananchi wenye sifa wanatakiwa kujitokeza kutimiza wajibu huo. Sifa hizo ni kuwa raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 na kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, awe na kadi ya mpiga kura.Pia awe mkazi wa eneo analotaka kupiga kura na jina lake liwe katika Daftari la Wapigakura. Wapigakura wanapaswa kufika katika kituo cha kupigaji kura kati ya 1:00 asubuhi hadi 10:00 jioni.

Baada ya kupiga kura unatakiwa:

1. Kuondoka eneo la kupigia kura

2. Kutokufanya kampeni ya aina yoyote kesho.

3. Kutovaa sare za chama cha siasa.

Utaratibu wa kupiga kura

Ufuatao ndio utakuwa utaratibu kwenye vituo vyote 899 vitakavyotumika kwa shughuli hiyo:

1.Vituo vitakuwa na wakala wa vyama vya siasa wakati wote wa zoezi la upigaji kura. Kituo kisipokuwa na wakala, Msimamizi wa kituo hazuiwi kuendelea na zoezi la kupiga kura.

2.Mpigakura atapiga kura katika kituo alichojiandikishia na atatakiwa kuonyesha kadi yake kama uthibitisho kuwa yeye ni mpigakura.

3.Kwa mpigakura mwenye ulemavu wa macho na asiyejua kusoma na kuandika ataruhusiwa kusaidiwa na mtu mwingine tofauti na msimamizi wa kituo, msimamizi wa kituo msaidizi na wakala wa chama, ili amsaidie.

4.Msimamizi wa kituo atahakiki jina la mpigakura kama lipo katika daftari la kituo hicho.

5.Mpigakura ataweka alama ya ‘V’ kwenye karatasi ya kura. Baada ya hapo ataikunja na ataitumbukiza ndani ya sanduku la kupigia kura.

Wanaoruhusiwa kuwepo kituoni

Sheria inawaruhusu watu wafuatao kuwapo katika kazi ya kuhesabu kura; msimamizi wa kituo na msaidizi wake, karani mwelekezaji, wakala wa chama cha siasa, mgombea, askari polisi au mtu mwingine anayehusika na usalama katika sehemu ambayo kura zinahesabiwa.

Wengine ni mjumbe wa tume, mkurugenzi wa uchaguzi au ofisa wa tume na mwangalizi

No comments:

Post a comment