Saturday, 24 February 2018

Hakuna mgomo! Majimaji wathibitisha. Yanga wajiandae


Beki kisiki wa timu ya soka ya Majimaji Jaffary Mohamed, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo ambao walikuwa wanadhani ya kuwa wachezaji wamegoma kuwa mambo yameshakuwa mazuri na watashuka kwa nguvu ile ile kwenye mechi ya kombe la Shirikisho dhidi ya Dar Young Africans.

Jaffary ambaye anasherehekea siku yake ya kuzaliwa, amesema kulikuwa na sintofahamu kwa siku mbili zilizopita hali iliyofanya kushindwa kuhudhuria vyema kwenye mazoezi lakini uongozi tayari umeshazungumza nao na mambo yanaenda vizuri wakijiandaa na mchezo huo utakaofanyika Jumapili kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.

“Wote tupo kambini timu nzima ipo kambini, kwa mimi ninavyoona kwa sasa hakuna mtu ambaye amegoma na maandalizi yanakwenda vizuri na sijaona mchezaji yoyote ambaye ameondoka kambini,”Jaffary ameeleza.
Kulikuwa na mgogoro.

“Kugoma kweli ilitokea siku mbili za nyuma, kulikuwa na migogoro ya hapa na pale lakini limeenda na kukaa sawa, mpaka jana (Ijumaa) tumeingia kambini wote na tumeendelea na mazoezi,” amesema.

Jaffary ambaye msimu uliopita aliichezea Toto Africans ya jijini Mwanza amesema Yanga wajiandae kukabiliwa na mchezo mgumu na wenye ushindani kwani wachezaji wamekuwa na morali kubwa ya kutaka kufuta aibu ya mechi ya ligi waliyofungwa kwa mabao 4-1.

“Mimi nashukuru wachezaji tumejiandaa vizuri, mpaka sasa hakuna wenye majeraha yatakayomuweka nje ya mchezo huo, tunaomba Mungu atujalie matokeo mazuri mechi yetu dhidi ya Yanga kwani sisi tunahitaji kusonga mbele kwenye kombe hili la Shirikisho, tutapambana kwa uwezo wetu wote, naomba tuachane na mambo haya yameshapita,” amesema.
Ilipoanzia

Kwa mujibu wa Gazeti la Mwanaspoti, ni kuwa wachezaji kadhaa wa Majimaji walikuwa wamejiengua kwenye kikosi kitakachocheza na Yanga kwenye raundi ya 16 bora ya michuano ya Azam Sports Federation Cup kushinikiza kulipwa fedha zao za usajili na mishahara.

Mwanaspoti ilienda mbali na kusema kuwa Kocha Habibu Kondo amekuwa akilalamika kuwa mpaka Ijumaa asubuhi alikuwa amebakiwa na kikosi cha pili pamoja na wachezaji wengine 14 kutoka timu ya vijana huku wachezaji wote muhimu wakiwa wamekimbia kambi hiyo.l
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: