MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wahitimu wa vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) kutumia ujuzi walioupata kujiajiri na kuanzisha shughuli za kiuchumi badala ya kusubiri kuajiriwa.

Akizungumza leo Novemba 12, 2026, katika mahafali ya 56 ya Chuo cha VETA Dar es Salaam, Chalamila amesema kuwa elimu ya ufundi stadi ni fursa ya kuwawezesha vijana kujitegemea kiuchumi na kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Amesema kuwa wahitimu wanapaswa kubadilisha changamoto zinazowazunguka kuwa fursa za kujipatia kipato, huku akiwataka wazazi kuacha kuwakatisha tamaa watoto wanaochagua elimu ya ufundi stadi kwa kuiona kama njia ya watu walioshindwa katika masomo.

“VETA siyo mahali pa kukimbilia walioshindwa, VETA ni mahali pa watu kuja kuwa na ndoto, kuzikuz­a ndoto na kuzifanya ndoto kuwa kweli,” amesema Chalamila.

Aidha, amesema kuwa Dar es Salaam ina fursa nyingi za kiuchumi kutokana na uwepo wa viwanda zaidi ya 1,000 na shughuli mbalimbali za biashara, hivyo wahitimu wanapaswa kutumia taaluma zao katika sekta hizo.

Pia amewataka wahitimu wa fani za mitindo ya mavazi, uchapishaji na ufundi wa magari kuanzisha biashara na huduma zinazohitajika katika soko, badala ya kusubiri nafasi za ajira.

Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kufuatilia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri kwa makundi ya wajasiriamali ili kupata mitaji ya kuanzisha na kukuza biashara zao.

Kwa upande mwingine, amewataka wahitimu watakaopata ajira kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa bidii, huku wakilinda mali za waajiri wao ili kujenga uaminifu na kuongeza nafasi za maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Dar es Salaam, Abraham Mbughuni, amesema kuwa chuo hicho kinakabiliwa na changamoto ya uchache na uchakavu wa vitendea kazi, hali inayokwamisha utoaji wa mafunzo kwa vitendo.

Aidha, amebainisha kuwa chuo kinahitaji mabasi mawili, malori mawili aina ya semi-trailer, magari 20 ya mafunzo ya udereva wa awali, mitambo ya forklift pamoja na vifaa vingine vya kufundishia.

Amesema kuwa kwa sasa chuo kina magari 11 ya mafunzo ya udereva wa awali yanayohudumia wanafunzi takribani 400 kwa mwezi, huku mahitaji yakiwa makubwa zaidi.


Pia ameongeza kuwa chuo kinakabiliwa na uhaba wa majengo, madarasa, samani na vifaa vya kisasa vinavyoendana na mabadiliko ya teknolojia.


Mbughuni amesema kuwa chuo hicho kina wahitimu 20 wenye mahitaji maalumu wanaohitaji mitaji na vifaa vya kuwawezesha kujiajiri, akimtaja mhitimu Francis aliyebuni chaja ya kompyuta mpakato na ambaye kwa sasa anatumika pia kama mkufunzi chuoni hapo.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: