WANANCHI 1,560 na mifugo 3,480 katika Kitongoji cha Katikati, Kijiji cha Njoroi, Kata ya Ololosokwan, Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha, wanatarajia kuondokana na adha ya kutembea zaidi ya kilomita saba kusaka maji kufuatia uzinduzi wa mradi wa maji wa Sh milioni 65.
Kabla ya kukamilika kwa mradi huo, wananchi walilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu,huku wengine wakivuka mpaka kwenda nchini Kenya, hali iliyokuwa ikiongeza mzigo kwa wanawake na watoto.
Mradi huo uliozinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Brigedia Jenerali Wilson Sakulo, unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya wananchi na mifugo, pamoja na kupunguza changamoto za kiusalama zinazohusiana na safari za kutafuta maji.
Naye Kaimu Meneja wa RUWASA, wilayani hapo, Jumbe Mollel, amesema Kitongoji cha Katikati kilikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji, ambapo RUWASA iliwahi kujaribu kupeleka mitambo kwa ajili ya kuchimba kisima, lakini juhudi hizo hazikufanikiwa.
Wakati huo huo, Mjumbe wa Bodi ya PWC, Kooya Timan, amewataka wanawake wanaonufaika na mradi huo kuutunza na kuhakikisha miundombinu yake inabaki katika hali nzuri ili huduma hiyo iendelee kutolewa kwa muda mrefu.


Post A Comment: