ARUSHA, Septemba 4, 2026 — Mafunzo ya siku nne ya Umahiri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Walimu Tanzania (ICT Competency Standards for Teachers in Tanzania - ICT CSTT) yameahirishwa leo jijini Arusha, huku walimu wakihimizwa kutumia maarifa na stadi walizojifunza kuboresha ufundishaji, ujifunzaji, tathmini pamoja na kuwawezesha waalimu wenzao.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Gold Crest Hotel kuanzia Septemba 1 hadi 4, 2026, yamewajengea washiriki uwezo wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Akili Bandia (AI), rasilimali za kidijitali na mifumo ya kujifunzia kwa njia ya mtandao katika kazi za kila siku za mwalimu.
Akifunga mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Bw. Mathias Innocent Mvula, amebainisha kuwa kukamilika kwa mafunzo hayo kunapaswa kuwa mwanzo wa utekelezaji wa maarifa na stadi hizo katika shule za na za jirani.
Kwa mtazamo wake, thamani ya uwekezaji huo itaonekana kupitia mabadiliko katika ufundishaji na ujifunzaji, badala ya kuishia kwenye vyeti. Amewataka washiriki kutekeleza mipango kazi waliyoandaa wakati wa mafunzo na kuonesha hatua watakazochukua katika utekelezaji wanaporejea shuleni.
Akieleza mazingira mapya ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la mwaka 2023, Bw. Mvula amebainisha kuwa maendeleo ya teknolojia, hususan Akili Unde, yamebadilisha namna watu wanavyopata taarifa na maarifa, hali inayohitaji walimu kuongeza uwezo wa kutumia zana hizo kwa malengo ya kuinua ubora wa elimu.
Amebainisha pia kuwa simu za mkononi na vifaa vingine vya kidijiti vinaweza kuwa nyenzo muhimu za kujifunzia na kufundishia vinapotumiwa kwa usahihi. Hata hivyo, matumizi ya teknolojia yanapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya sera na mitaala yanayolenga kujenga umahiri wa mwanafunzi.
Kwa mujibu wa Bw. Mvula, elimu ya sasa inalenga kumwandaa mwanafunzi kutumia maarifa na stadi katika maisha halisi, kukabiliana na changamoto na kutumia fursa za kiuchumi, badala ya kutegemea ajira pekee. Ameeleza kuwa kuimarishwa kwa mikondo ya amali ni miongoni mwa hatua zinazolenga kuongeza uwezo huo.
Katika kuendana na mabadiliko hayo, Bw. Mvula ametoa wito kwa walimu kuendelea kutumia fursa za Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA), akibainisha kuwa ujifunzaji kwa njia ya mtandao unawapa nafasi ya kuongeza uwezo kitaaluma na kitaalamu bila kulazimika kurejea chuoni mara kwa mara.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuweka mifumo endelevu ya kuimarisha umahiri wa walimu, ikiwemo utaratibu wa kutambua mafunzo kabilishi mbalimbali ya kuwajengea uwezo walimu ili kuboresha elimu nchini.
MKOA WATAKA UJUZI UONEKANE SHULENI
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Elimu Mkoa wa Arusha, Bw. Vicent Boniface Kayombo, amewataka walimu walioshiriki katika mafunzo hayo kuwa kiungo cha kusambaza maarifa kwa walimu wenzao na kuhakikisha ujuzi walioupata unatafsirika katika vitendo vya ufundishaji na ujifunzaji shuleni.
Kayombo ameeleza kuwa Mkoa wa Arusha una mpango wa utekelezaji wa MEWAKA katika shule za msingi na sekondari, hivyo walimu walioshiriki katika mafunzo hayo wana nafasi muhimu ya kusaidia kufanikisha mpango huo kwa kushirikisha wenzao na kuchochea matumizi yenye tija ya TEHAMA katika shule zao.





Post A Comment: