Serikali imesisitiza kuwa inaendea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba katika ngazi ya Afya ya Msingi,  ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Silas Shemdoe (Mb.), wakati akitoa salamu za ofisi yake katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Afya ya Msingi unaofanyika Arusha jijini Arusha katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC).

Prof. Shemdoe amesema takwimu za mwaka 2025 zinaonesha umuhimu mkubwa wa vituo vya Afya ya Msingi, ambapo kati ya wajawazito milioni 2.09 waliojifungulia katika vituo vya afya vya umma, milioni 2 sawa na asilimia 95.6 walipata huduma katika ngazi hiyo.

Aidha, amefafanua kuwa kati ya mahudhurio milioni 32.3 ya wagonjwa wa nje katika vituo vya umma, milioni 27.8 sawa na asilimia 86 yalifanyika katika vituo vya Afya ya Msingi.

Amesema kati ya vituo 8,288 vya afya vya Serikali nchini, vituo 7,946 sawa na asilimia 95.8 ni vya ngazi ya Afya ya Msingi vinavyomilikiwa na Halmashauri.

Kwa upande wa TEHAMA, Prof. Shemdoe amesema asilimia 96.6 ya vituo hivyo vimeunganishwa na mfumo wa GoTHOMIS, huku asilimia 87.6 vikiwa vimeunganishwa na GePG, hatua inayosaidia kuongeza ufanisi, uwazi na usimamizi wa mapato na huduma.

"Ninaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha sekta ya Afya nchini kwa uwekezaji mkubwa unaondelea katika ngazi ya Afya ya Msingi," ameeleza  Prof. Shemdoe.

Prof. Shemdoe ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya usimamizi wa dawa na bidhaa za afya ili kuhakikisha upatikanaji wake unaimarika katika vituo vya kutolea huduma.

Prof. Shemdoe ameahidi kuimarisha usimamizi na uwajibikaji kupitia Mikoa, Wilaya na Halmashauri ili kuhakikisha uwekezaji unaofanywa na Serikali unaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

Mkutano huo unaofanyika Septemba 09 hadi 11, 2026 umefunguliwa na Mhe. Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba kwa niaba ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu, umelenga kujadili namna ya kuimarisha huduma za Afya ya Msingi, ugharamiaji endelevu, ufanisi, ubora wa huduma na mifumo imara ya afya ili kufikia lengo la  Afya kwa Wote.












Share To:

Post A Comment: