PEMBA — Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Bw. Khamis Abdulla Said, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kuendelea kufadhili miradi ya maendeleo ya elimu Unguja na Pemba, akisema hatua hiyo inasaidia kuboresha mazingira ya ujifunzaji na kuinua ubora wa elimu visiwani humo.
Bw. Said ameyasema hayo wakati akiongoza ziara ya ukaguzi wa miradi inayofadhiliwa na TEA Kisiwani Pemba, akifuatana na Mkurugenzi Mkuu wa TEA Dkt. Erasmus Fabian Kipesha, ujumbe wa taasisi hiyo pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Katika ziara hiyo, viongozi hao walikagua miradi mbalimbali katika Maktaba Kuu ya Pemba, Skuli ya Madungu pamoja na ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Amali Kangagani Wilayani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa lengo la kutathmini maendeleo na hali ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa upande wake Dkt. Kipesha amesema, ameridhishwa na ubora wa miradi hiyo akieleza kuwa hali yake inaakisi thamani halisi ya uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya elimu.
Amesema, usimamizi mzuri unaofanywa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar umechangia katika utekelezaji mzuri wa miradi iliyokamilika na inayoendelea.
Dkt. Kipesha ametoa rai kwa wahusika kuhakikisha miradi yote inayoendelea inakamilishwa kwa wakati ili ianze kutumika na kusaidia kupunguza changamoto za miundombinu ya elimu katika maeneo husika.












Post A Comment: