NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa wito wa kujenga mifumo itakayowezesha ubunifu na fursa za mazingira kugeuzwa kuwa miradi inayotekelezeka, inayoweza kufadhiliwa na kukua.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira wa NEMC, Dkt. Careen Kahangwa, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, wakati wa kufunga Mkutano wa Tanzania Green Summit 2026 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kahangwa amesema mfumo huo unapaswa kuwaunganisha wabunifu, wajasiriamali na jamii na ujuzi, teknolojia, masoko, taasisi za fedha pamoja na washirika wa maendeleo.
Amesema mawazo mazuri hayapaswi kubaki katika mashindano, maonesho au miradi ya majaribio pekee, bali yanapaswa kubadilishwa kuwa biashara endelevu, ajira, uwekezaji na suluhisho la changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, ametoa wito wa kujenga ushirikiano wa kudumu utakaosaidia kutafsiri maazimio ya mkutano huo kuwa hatua na matokeo yanayopimika.
Amesema Tanzania Green Summit haipaswi kuwa tukio la siku mbili pekee, bali iwe sehemu ya mchakato endelevu wa kuunganisha sera, ubunifu, fedha, teknolojia na utekelezaji.
Dkt. Kahangwa pia amesisitiza umuhimu wa kufuatilia fursa zilizojadiliwa, kuendeleza ushirikiano ulioanzishwa na kupima matokeo ya hatua zitakazochukuliwa baada ya mkutano huo.
Mkutano wa Tanzania Green Summit 2026 ulifanyika Septemba 15 na 16, 2026, ukiwa na kaulimbiu “Turning Climate Action into Opportunity”, yenye maana ya “Kugeuza Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kuwa Fursa.”

Post A Comment: