Mwenyekiti wa Vijana wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, CPA (T) Yuvenali Shirima, amewataka wananchi kuchukua tahadhari na kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa katika msimu wa Vuli 2026.

Shirima amewataka wananchi kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kuzingatia maelekezo ya Serikali na wataalamu, pamoja na kuepuka maeneo hatarishi kama mabonde, maeneo ya mito na sehemu zenye miteremko mikali.

Aidha, ameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kujiandaa na kukabiliana na athari za El Niño, akisisitiza kuwa maandalizi ya mapema ni muhimu katika kulinda maisha, mali na miundombinu.

Katika pongezi hizo, amemtaja pia Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Godfrey Eliakimu Mzava, kwa juhudi zake za kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari. Amesema katika matukio mbalimbali, Mhe. Mzava amekuwa akitoa elimu kwa wananchi, kuitisha vikao na kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha jamii inaelewa namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.

“Tunampongeza Mkuu wa Wilaya kwa kuwa karibu na wananchi na kuendelea kutoa elimu. Elimu, tahadhari na maandalizi ya mapema vinaweza kusaidia kuokoa maisha na mali za wananchi,” amesema Shirima.

Amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali, kutoa taarifa za viashiria vya hatari na kuhakikisha wanachukua hatua stahiki kabla ya madhara kutokea.







Share To:

Post A Comment: