SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limehimiza wajasiriamali kuchangamkia fursa ya kuthibitisha ubora wa bidhaa wanaozalisha bure kwa gharama za Serikali, hatua ambayo itawasaidia kuondokana na vikwazo vya kiabiashara.

Mbali na wito huo kwa wajasiriamali, shirika hilo limewataka wananchi kuhakikisha wananunua na kutumia bidhaa zilizothibishwa ubora na shirika hilo kwa kujenga utamaduni wa kusoma taarifa zilizopo kwenye vifungashio.

Wito huo umetolewa na Meneja wa TBS Kanda ya Kaskazini,, Yona Afrika,. wakati akizungumza kwenye Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Arusha.

Alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wajasiriamali katika kukuza uchumi wa Taifa na wao binafsi, ndiyo maana imebeba dhamana ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zao bure.

"Kwa hiyo tumeshiriki katika maonesho haya kwa sababu ni fursa ya kukutana na wadau mbalimbali na kuwaelezea shughuli zinazofanywa na TBS na fursa nyingine ambazo zinapatikana kama kuthibitisha bidhaa za wajasiriamali bure," alisema.

Alisema bidhaa zikishathibitishwa na TBS zinaingia masoko ya Nchi za Afrika Mashariki (EAC) na ya kikanda bila vikwanzo vya biashara.

Alisema nchi za EAC zimeingia makubaliano, ambapo bidhaa zikishathitishwa na shirika la viwango la nchi husika,hazitakiwi kupimwa tena zinapopelekwa kwenye soko la nchi nyingine.

"Kwa hiyo TBS tumeshiriki maonesho haya kusudi kukutana na wadau mbalimbali, ambao tunawafikia na kuwapa taratibu za kufuata kuthibitisha ubora.

"Kwa kweli tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuandaa Maonesho haya ya Nanenane, kwani fursa muhimu ya kukutana na kutoa elimu kwa wadau.

Mfano tunawaambia kuwa wakipata barua ya utambulisho kutoka SIDO wakija kwetu utaratibu wa kuthibitisha ubora wa bidhaa unaanza mara moja, kwa wajasiriamali" alisema Afrika.

Kwa upande wa wananchi waliotembelea banda la TBS, walitakiwa kuhakikisha wanatumia bidhaa zilizothibitishwa ubora ili kulinda afya zao na kuona thamani ya fedha zao.

Alisema ni muhimu kusoma taarifa zilizopo kwenye vigungashio ili kujua kama zina ubora uliothititishwa na shirika pamoja na muda wake wa mwisho wa matumizi.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: