Na Mwandishi Wetu
Tanzania imeendelea kupiga hatua katika sekta ya afya ambapo kipimo kipya cha UTI kinachomwezesha mtu kujipima akiwa nyumbani na kugundua kuwa amepata maambukizi ya ugonjwa huo kimeanza kutumika hapa nchini.
Kipimo hicho kinachojulikana kama Checkfor UTI Test kimekuwa nyenzo muhimu kwani maambukizi ya njia ya mkojo, yanayojulikana zaidi kama UTI, ni miongoni mwa changamoto za kiafya zinazowakumba watu wengi katika jamii.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na daktari Dk Eshton Nkala wakati akizungumzia kipimo hicho kipya cha aina yake kuanza kutumika nchini.
Alisema mara nyingi, maambukizi haya huanza kwa dalili ambazo zinaweza kuonekana kuwa ndogo, ikiwemo kukojoa mara kwa mara, maumivu au muwasho wakati wa kukojoa, maumivu ya chini ya tumbo, mkojo kubadilika rangi au kuwa na harufu isiyo ya kawaida.
Alisema changamoto kubwa katika udhibiti wa UTI ni kuchelewa kutambua dalili na kuchelewa kufika katika vituo vya afya kwa uchunguzi na matibabu.
Aidha, alisema wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza kuwa utambuzi wa mapema ni hatua muhimu katika kupunguza uwezekano wa maambukizi kuongezeka, kujirudia mara kwa mara au kusababisha madhara zaidi kiafya.
Alisema katika kuimarisha hatua za awali za kujitambua, Checkfor UTI Test imeleta njia rahisi ya kumsaidia mtu kupata taarifa za awali kuhusu uwezekano wa kuwa na UTI akiwa nyumbani.
Alisema kipimo hicho hakichukui nafasi ya daktari au hospitali, bali kinamsaidia mtumiaji kuchukua hatua mapema pale anapokuwa na dalili au shaka kuhusu afya yake.
Alisema matokeo ya awali yanayopatikana kupitia kipimo hiki yanaweza kumsaidia mtu kufanya uamuzi sahihi wa kufika kituo cha afya kwa ajili ya ushauri wa kitaalamu, vipimo zaidi na matibabu stahiki.
“Hii ni muhimu hasa kwa watu ambao huchelewa kutafuta huduma za afya kwa sababu ya hofu, usumbufu, muda au kutokutilia maanani dalili za mwanzo,” alisema.
Aidha, alisema kipimo cha Checkfor UTI Test kinazalishwa nchini Tanzania na kampuni ya Canadian Biotech, jambo linaloonyesha mchango wa viwanda vya ndani katika kuunga mkono upatikanaji wa vifaa vya afya vinavyosaidia jamii kujitambua mapema na kuchukua hatua kwa wakati.
“Kipimo hiki kinaonesha ni kwa namna gani nchi inapiga hatua katika uzalishaji wa vifaa tiba na vifaa tiva hivi vinapatikana kupitia wasambazaji wake ambao ni JD Pharmacy, Bariki Pharmacy na Cugra General Supplier,” alisema na kuongeza.
“Katika zama ambazo huduma za afya zinahimizwa kuanza na uelewa wa mtu binafsi, Checkfor UTI Test ni nyenzo muhimu ya kusaidia utambuzi wa awali. Ujumbe wake ni wa afya ya umma: dalili zisipuuzwe, utambuzi ufanyike mapema, na matibabu sahihi yatafutwe kwa wakati,” alisema.



Post A Comment: