Serikali imeendelea kuimarisha jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia upatikanaji wa mitaji, mafunzo na masoko ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya Taifa. 

Hayo yameelezwa leo Juni 17, 2026 bungeni na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi alipokuwa akijibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga (Viti Maalum) aliyetaka kufahamu mipango maalum ya Serikali katika kuwawezesha wanawake.

Akijibu swali hilo, Mhe. Mahundi amesema Serikali inatumia mifumo mbalimbali ya uwezeshaji inayotekelezwa kupitia Wizara za kisekta pamoja na mamlaka za serikali za mitaa ikiwa na lengo la kuhakikisha wanawake wanapata fursa za kujenga uwezo wa kiuchumi, kuongeza kipato na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.

Amefafanua kuwa miongoni mwa mipango hiyo ni utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake huku kabla ya kunufaika na mikopo hiyo, wanawake hupatiwa mafunzo ya kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha kupitia ushirikiano kati ya Serikali, SIDO, VETA na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na maendeleo ya wanawake.

Naibu Waziri huyo pia amesema Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Jenga Kesho Yako (BBT) katika sekta za kilimo, mifugo na ufugaji nyuki, ambayo imekuwa ikitoa fursa kwa wanawake kujikita katika shughuli za uzalishaji mali ambayo imeendelea kuwajengea uwezo wa kiufundi na kuwasaidia kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na sekta hizo muhimu.

Katika sekta ya madini, Mhe. Mahundi amesema Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linaendesha programu maalum zinazowawezesha wanawake kushiriki katika shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kwa kuwapatia mafunzo, maarifa na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za uwekezaji. Hatua hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo yenye mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa.

Aidha, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kuimarisha huduma jumuishi za kifedha zinazowawezesha wanawake kupata mitaji kupitia SACCOS na kuboresha mazingira ya uwezeshaji wa wanawake ili kuhakikisha wanapata mitaji, mafunzo na masoko ya uhakika yatakayowasaidia kukuza biashara zao na kuchangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Share To:

Post A Comment: