Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka (Mb), amewataka wataalamu wa maendeleo ya jamii nchini kutumia taaluma, mbinu na uzoefu wao kuwaelimisha wananchi kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kuhakikisha kila Mtanzania anaielewa na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.

Mhe. Nanauka ametoa wito huo, alipokuwa akifungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA), uliofanyika katika Ukumbi wa Kwatunza Beach Arena, jijini Mwanza, leo Juni 17, 2026.

“Nyinyi mnazo mbinu na maarifa ya kuijenga jamii. Nendeni kwa wananchi mkawape elimu na uelewa kuhusu Dira ya Taifa 2050 ili wawe sehemu ya safari ya maendeleo ya nchi yetu,” amesema Mhe. Nanauka.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, amewahimiza wataalamu wa maendeleo ya jamii kuendelea kujiendeleza kitaaluma kwa kujiunga na programu ya Shahada ya Uzamili kwa njia mseto (Blended/Online) inayotolewa na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD), ambayo hukamilika ndani ya mwaka mmoja.

Aidha, Wakili Mpanju ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa wataalamu wa maendeleo ya jamii kupitia utoaji wa vitendea kazi, kuboresha maslahi ya kada hiyo na kuendelea kutoa ajira kwa wataalamu nchini.

Mkutano huo wa siku tatu unaendelea kesho kwa uwasilishaji wa mada mbalimbali zitakazotolewa na wataalamu na wadau wa maendeleo ya jamii, zikiwa na lengo la kuimarisha taaluma na mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa.
















Share To:

Post A Comment: