WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu) Profesa Palamagamba Kabudi ameta taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2025 ambapo inaonesha namna Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ilivyowekeza na kuweka nguvu kubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Akiwasilisha taarifa hiyo leo Mei 29,2029 Bungeni Mjini Dodoma ,Profesa Kabudi amesema uwasilishaji wa taarifa hiyo ni utekelezaji wa Kifungu cha 66 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015, inayoiagiza Serikali kuandaa na kuwasilisha bungeni taarifa hiyo kila mwaka.

“Lengo ni kuonesha uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi kupitia Bunge, pamoja na kutoa tathmini ya utekelezaji wa mikakati ya udhibiti wa dawa hizo kwa mwaka husika.Pia, taarifa hii inatoa nafasi kwa Bunge kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu namna bora ya kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya nchini.”

Amefafanua kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vyombo vya ulinzi na usalama, wadau wa ndani na nje ya nchi pamoja na jamii kwa ujumla, serikali imepata mafanikio makubwa katika kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya.Katika taarifa hiyo Profesa Kabudi amesema mwaka 2025, bangi iliendelea kuwa dawa ya kulevya iliyokamatwa kwa kiwango kikubwa zaidi ambapo jumla ya tani 1,017.26, zilikamatwa.

Amefafanua hata hivyo, kiasi kilichokamatwa kilipungua kwa asilimia 55.97 ikilinganishwa na mwaka 2024.Hiyo ni kutokana na uteketezaji wa mashamba makubwa ya bangi uliofanyika mwaka 2024 na kuimarika kwa udhibiti ikiwemo utoaji elimu kwa jamii inayojihusisha na kilimo cha bangi kuhusu madhara ya kilimo cha zao hilo.

Ameongeza pia jumla ya tani 26.36 za mirungi zilikamatwa. Kiasi hicho kiliongezeka kwa asilimia 42.88 ikilinganishwa na mwaka 2024. Ongezeko hilo linaashiria kuimarika kwa operesheni za ufuatiliaji na udhibiti hususan katika maeneo ya mipaka na njia zinazotumika kusafirisha dawa hizo.

Kwa upande wa dawa za kulevya za viwandani, amesema Serikali ilifanikiwa kukamata methamphetamine kilogramu 907.18, heroin kilogramu 672.23, cocaine kilogramu 4.89, MDMA gramu 178 na MDA gramu 7.82.

Aidha, kwa mara ya kwanza, mwaka 2025 Serikali ilikamata tani 29.52 za aina mpya ya dawa za kulevya aina ya Kratom itokanayo na mmea unaoitwa Mitrogyna speciosa. “Dawa hii iliingizwa nchini kama mbolea, baada ya uchunguzi ilibainika kuwa ni dawa za kulevya.”

Amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama katika kudhibiti mitandao na njia za usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia Nchi kavu, anga na majini.

Aidha, Serikali iliendelea kuimarisha ukaguzi katika vituo vya forodha, vyombo vya usafiri, kampuni za usafirishaji vifurushi na kwenye kampuni zinazojihusisha na biashara ya kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya kwa lengo la kudhibiti uchepushwaji.

“Kupitia ukaguzi huo, jumla ya tani 31.76 na lita 183.500 za kemikali bashirifu pamoja na kilogramu 2.36 na mililita 160 za dawa tiba zenye asili ya kulevya zilikamatwa.”

Kuhusu makosa ya dawa za kulevya, mwaka 2025,amesema jumla ya mashauri 1,124 yalifunguliwa katika Mahakama mbalimbali nchini. Pamoja na mashauri yaliyokuwa yakiendelea katika Mahakama mbalimbali nchini, mashauri 1,373 yalitolewa hukumu na Jamhuri ilishinda mashauri 1,058.

Aidha mali zenye thamani ya zaidi ya Tsh. bilioni 3.3 zilizohusishwa na makosa ya dawa za kulevya zilitaifishwa.Pia Serikali iliendelea kutoa huduma za tiba na utengamao kwa watu wenye uraibu wa dawa za kulevya.

“Mwaka 2025, jumla ya watu 85,425 wenye uraibu wa dawa za kulevya walipata tiba kwenye vitengo vya afya ya akili katika hospitali za rufaa za mikoa na Kanda, kliniki za MAT na nyumba za upataji nafuu nchini.

“Elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya iliendelea kutolewa kwa Umma kupitia kampeni mbalimbali za uelimishaji katika jamii, taasisi za elimu na vyombo vya habari ili kuijengea jamii uelewa, maamuzi sahihi na uwezo wa kujilinda dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

“Katika kuimarisha ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia, kujenga uwezo wa kitaasisi pamoja na kuendesha operesheni za pamoja dhidi ya mitandao ya usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.

“Matokeo chanya katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanatokana na dhamira thabiti, maono na uongozi mahiri wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani chini ya uongozi wake amewekeza kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya Nchini.”

Pia ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama, wataalamu wa afya, wadau katika mapambano na wananchi kwa ushirikiano wao uliosaidia kuyafikia mafanikio aliyoyaeleza.

“Naomba wananchi waendelea kutoa taarifa pale wanapohisi au kushuhudia viashiria vya biashara au matumizi ya dawa za kulevya kwa vyombo husika ili kuifanya nchi yetu kuwa mahali salama na huru dhidi ya matumizi na biashara dawa za kulevya.”
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: