Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza kasi katika utafiti wa upatikanaji wa maeneo mapya ya uchimbaji wa visima vipya vya gesi asilia ili kuongeza upatikanaji wa gesi kwa matumizi mbalimbali pamoja na kufanikisha agenda ya matumizi ya nishati safi nchini.
Ndejembi ameeleza hayo tarehe 27 Februari 2026 mkoani Mtwara wakati akizindua mradi wa uchimbaji wa visima vitatu ambapo viwili ni kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay na kimoja kwa ajili ya utafutaji huku utekelezaji umefikia asilimia 58.
“Rai yangu kwenu TPDC ni kuongeza kasi ya uchimbaji wa gesi katika maeneo mengine na kuhakikisha mashapo yaliyopo yanaanza kuzalisha tunapozindua kitalu hiki hapa mipango ya kuanza kuchimba sehemu nyingine ianze mara moja” amesisitiza Ndejembi.
Ndejembi ameeleza kuwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan iliamua kuwekeza fedha kupitia TPDC kwani mahitaji ya gesi yanaongezeka kutokana na nchi inavyoendelea kukua na kusababisha mahitaji ya gesi kuongezeka kwa ajili ya uzalishaji wa umeme matumizi ya viwandani na taasisi nishati kwenye vyombo vya usafiri pamoja na matumizi ya majumbani.
Ndejembi ameipongeza TPDC kwa kushirikiana na Kampuni ya Maurel & Prom katika kutekeleza mradi wa uchimbaji wa visima hivyo ambavyo vitaongeza uzalishaji wa gesi na kuchochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi.
Kadhalika Ndejembi ameitaka TPDC kuendelea kuyawezesha makampuni na wataalamu wazawa ikiwa ni pamoja na kuweka mpango wa kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu waliopo katika maeneo ya utekelezaji wa miradi ili nao wanufaike na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi yao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Dkt James Mataragio ameeleza kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika nishati ya gesi ambapo katika mradi huo pekee itatumika zaidi ya shilingi bilioni 235.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mussa Makame amesema Serikali kupitia TPDC inamiliki Kitalu cha Mnazi Bay kwa asilimia 40 na Kampuni ya Maurel & Prom inamiliki asilimia 60 na kubainisha kuwa uzalishaji umeendelea kuongezeka ambapo kwa sasa uzalishaji katika kitalu hicho umefikia futi za ujazo milioni 100 kwa siku.

Post A Comment: