Na Denis Chambi, Tanga.
MGOMBEA wa nafasi ya Urais kupitia chama cha Alliance Democratic Change (ADC) Wilson Elias Mulumbe ameahidi Serikali atakayoiongoza itahakikisha inarejesha viwanda vyote vilivyobinafsishwa pamoja na kufufua vilivyokufa ili viweze kuzalisha na hatimaye kuwapatia wananchi ajira za kudumu hatua ambayo itainua uchumi wa mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika mwendelezo wa kampeni zake mkoani Tanga Mulumbe amesema kuwa kutokana na ubinafsishwaji wa viwanda na vingine vikashindwa kuendelea kuzalisha kumechangia kwa kiasi kikubwa ukosefu wa ajira hususani kwa vijana ambao ndio Nguvu kazi ya Taifa.
Ameongeza kuwa pamoja na kuvirejesha viwanda hivyo ikiwemo vilivyokuwepo mkoani Tanga pia atahakikisha anajenga kiwanda cha kuchakata Samaki ambao watakuza soko la ndani na nje ya nchi huku akiahidi kukaa upya na wawekezaji ambao walifunga viwanda vyao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kodi kuwataka wavifungue ili waweze kuzalisha ajira kwa watanzania.
" Wenzetu baada ya kubinafsisha viwanda hivi walitakiwa kuvisimamia lakini mwisho wa siku waliwaachia mabepali ambao waliviua, ahadi yetu kwa wananchi ni kwamba sasa tunaenda kuvifufua na kuvirudisha mikononi mwa Serikali na vijana wetu wataenda kufanya kazi"
"Viwanda vingi hapa Tanga vilifungwa kutokana na wingi wa kodi ambazo wawekezaji wameshindwa kulipa kwenye mamlaka lakini sisi tutakapoingia madarakani tutawaita na kukaa nao wawekezaji wote ambao walifunga viwanda vyao waendelee kufanya kazi ili kuzalisha ajira kwa watanzania" amesema na kuongeza
"Naomba mtuchague chama cha ADC ili viwanda vingi vilivyokufa ikiwemo kiwanda Cha Amboni tutakifanya kuwa kiwanda Cha kuchakata minofu ya Samaki na kutengeneza nyenzo za uvuvi wa Samaki ili kila mwezi tuweze kuvua tani 40 za Samaki ambazo zitachakatwa na kupelekwa kwa walaji wa ndani na nje ya nchi yetu" amesema Mulumbe.
Mbali na hayo Mulumbe ameahidi endapo atachaguliwa October 29 kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Serikali yake itahakikisha inawalipa mishahara wenyeviti wa Serikali za mitaa ,vijiji na vitongoji ili kuwawezesha na kuwapa motisha ya kufanya kazi.
"Hata wenyekiti wetu wa Serikali za mitaa tutaweza kuwalipa mishahara mbali na kazi kubwa wanayoifanya lakini bado Serikali iliyopo madarakani haiwalipi chochote endapo mkitupa ridhaa ya kuiongoza hii nchi kuanzia mwishoni mwa mwaka huu wa 2025 tutaanza kuwalipa mishahara hapo ndio wakati ambapo watafanya kazi kwa uadilifu na kuweza kuwasaidia wananchi wetu" ameongeza mgombea huyo.
Awali akizungumza mwenyekiti wa Alliance Democratic Change 'ADC' Taifa Shabani Itutu ameeleza kero za wananchi ambazo zimekuwa zikielekezwa kwa Mahakama ma Jeshi la Polisi nchini ambapo amesema kuwa utoaji wa haki umekuwa ukighubikwa na vitendo vya rushwa jambo ambalo limekuwa likiwanyima haki wanaostahili.
"Kuna malalamiko mengi ya wananchi juu ya Jeshi la Polisi unapopelekwa kituo chochote cha Polisi huwezi kutoka bila ya chochote hii sii haki kabisa wengine ni watu wa Mahakama shida imekuwepo kwenye utoaji wa hukumu watu wengi wenye maisha ya chini wanalalamika hawapati haki mpaka watoe rushwa tuwaambie tu kwamba nchi hii inafuata misingi ya sheria na katiba ya nchi dhamana ni haki ya kila mtu na kupata haki ni haki ya kila mtu"
Aidha chama hicho cha Alliance Democratic Change (ADC) kimetumia kampeni hizo kumnadi mgombea ubunge kupitia chama cha Wananchi CUF wa Jimbo la Tanga Mussa Mbarouk ikiwa ni ishara ya kumuunga mkono na kumuombea kura kwa wananchi ifikapo October 29 mwaka huu kwenye uchaguzi mkuu wa madiwani ,wabunge na Rais.
MWISHO.
Post A Comment: