Serikali wilayani Mbulu kwa kushirikiana na Taasisi ya Kifedha ya CRDB imewataka maafisa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii kuwasaidia vikundi vya wanawake, vijana na makundi maalum vinavyohitaji mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, maarufu kama fedha za Mama Samia, hususan vile ambavyo vimeshindwa kutimiza vigezo vya kupata mikopo hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu, wakati wa uzinduzi rasmi wa utoaji wa mikopo hiyo kwa vikundi 20 vilivyopata fursa ya kunufaika katika awamu hii.
“Jukumu la maafisa maendeleo ya jamii halipaswi kuishia tu kwenye kusimamia utoaji wa mikopo. Tunahitaji wajenge uwezo wa vikundi, wawatembelee, wawashauri na kuwasaidia pale wanapokumbwa na changamoto ili kuhakikisha wanapiga hatua,” alisema Michael Semindu, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu.
Katika awamu hii, kiasi cha shilingi milioni 120 kimetengwa kwa ajili ya mikopo hiyo, ambapo vikundi 15 ni vya wanawake, vitatu vya vijana, na viwili vinahusisha makundi maalum.
Kwa upande wake, Meneja wa Biashara wa Kanda ya Kaskazini kutoka benki ya CRDB, Emmanuel Kafui, amesema benki hiyo inatamani kuona vikundi hivi vikijengeka na kuanza kufanya shughuli zao kwa weledi wa kibiashara, huku wakitumia fursa hiyo kuingia rasmi kwenye mifumo ya kifedha nchini.
“CRDB tunataka kuona haya makundi yanajisimamia, yanakua kibiashara, na baadaye yanaweza hata kukopesheka kupitia taasisi za kifedha kwa utaratibu wa kawaida,” alisema Kafui.
Naye Zainabu Moshi, mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo, ameishukuru serikali kwa fursa hiyo akisema imemsaidia kuondokana na hali ya utegemezi na kumpa dira mpya ya maisha.
“Tulikuwa hatuna pa kuanzia, lakini kwa mkopo huu tunaweza kuanzisha biashara ndogo ndogo na hatimaye kuwa huru kiuchumi,” amesema Zainabu.
Mikopo hiyo inayotolewa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri inalenga kuwakwamua wananchi kutoka kwenye umaskini kwa kuwapa mitaji ya kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Post A Comment: