Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Shigeki Komatsubara, amefanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Njombe yenye lengo la kutembelea na kujionea fursa za uwekezaji zilizopo Mkoanj Njombe, hasa zile zilizojikita zaidi kwenye  mazao ya kilimo na kuongeza thamani.

Mara baada ya kuwasili, Bw. Komatsubara alipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ambaye alitumia nafasi hiyo kumkaribisha mkoani Njombe na kumweleza  fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta mbalimbali.

“Mkoa wa Njombe una ardhi nzuri na yenye rutuba, mazingira rafiki kwa uwekezaji, na wananchi wachapakazi. UNDP mnayo nafasi ya kipekee ya kushirikiana nasi katika kuinua kilimo, viwanda na ajira kwa vijana wetu,” alisema Mhe. Mtaka.

Katika ziara hiyo, Bw. Komatsubara alitembelea viwanda mbalimbali vikiwemo cha kuchakata mafuta ya parachichi cha AVO Afrika, kiwanda cha kufungasha parachichi Makambako, kiwanda cha mbao cha EAST KELIN WOOD, pamoja na viwanda vya chai vya Kibena na TANWAT.

Akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, alipewa taarifa ya fursa za uwekezaji zilizopo mkoani humo, hasa katika sekta ya kilimo, viwanda vidogo na huduma za kijamii.

Akizungumza mwishoni mwa ziara yake, Bw. Shigeki Komatsubara jana tarehe 11, 2025 alisema:

“Nimefurahishwa sana na mapokezi niliyoyapata Njombe. Ardhi yenye rutuba, mazingira mazuri na watu wa kujituma vinaufanya mkoa huu kuwa na fursa kubwa sana za maendeleo. Bila shaka, nitarejea tena Njombe kuona namna bora ya kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya pamoja.”

Ziara hii inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya UNDP na Serikali ya Mkoa wa Njombe katika kuchochea maendeleo endelevu kupitia uwekezaji, ubunifu, na matumizi bora ya rasilimali zilizopo.












Share To:

Post A Comment: