Na. Saidina Msangi, WF, Arusha.

Watumishi wa Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali wamehimizwa kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na kujituma kwa kuwa ni daraja muhimu kati ya usimamizi wa fedha za umma na mafanikio ya maendeleo ya wananchi.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Huduma za Hazina, Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, wakati akifungua Mkutano wa Watumishi wa Idara hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Olasite Garden, jijini Arusha.

Alisema mkaguzi wa ndani si tu mtathmini wa taarifa za kifedha, bali ni mshauri wa usimamizi bora, anayechangia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha taasisi zinafanya kazi kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia misingi ya sheria, taratibu na kanuni.

‘‘Mafanikio tunayoyaona katika usimamizi wa rasilimali za umma na thamani ya pesa katika miradi ya maendeleo yanaonesha kazi kubwa na juhudi zinazofanywa na wakaguzi wa ndani kutoka katika taasisi za Serikali. Juhudi hizi zinapaswa kuendelezwa kwa kasi zaidi ili nchi yetu iendelee kupiga hatua zaidi za maendeleo chini ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan’’, alisema Bi.Omolo.

Aidha, Bi. Omolo aliwasisitiza kuhusu umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha, kutambua mapema maeneo yenye viashiria hatarishi, na kutoa mapendekezo yanayotekelezeka kwa wakati.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuthamini mchango wao na itaendelea kuweka mazingira bora ya kazi kwa kuhakikisha wanapata mafunzo, vifaa na msaada unaohitajika ili kutimiza majukumu yao kwa weledi.

‘‘Katika mazingira ya sasa ambapo Serikali inaendelea kusisitiza mageuzi ya kiutendaji, mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, nafasi yenu ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote, wakaguzi wa ndani mna jukumu la kuwa walinzi wa maadili, waangalizi wa utendaji, na washauri wa maboresho ya mifumo ya ndani’’, alisisitiza Bi. Omolo.

Pia Bi. Omolo aliwasisitiza kuweka mikakakati ya kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wakaguzi ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Bw. Benjamin Magai alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kujadili utekelezaji wa majukumu ikiwemo mafanikio na changamoto ili kuangalia namna ya kuboresha utendaji kazi.

‘’Katika kutekeleza shughuli zetu kuna mafanikio ambayo tumeyapata ikiwemo usimamizi wa taasisi za umma kuona utendaji kazi wao na kutoa uelewa kwa taasisi mbalimbali kuhusu usimamizi wa vihatarishi, kufanya uthibiti katika taasisi mbalimbali, kufanya kaguzi za kiufundi na ufanisi na kaguzi maalumu ‘’, alisema Bw. Magai.

Bw. Magai aliongeza kuwa Idara hiyo itaendela kuwajengea uwezo watumishi wake ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Mkutano huo umewakutanisha watumishi wa Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali kwa lengo la kujadili mafanikio, changamoto, na njia bora za kuboresha utendaji kazi kwa manufaa ya umma kwa kuhakikisha uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali za umma










Share To:

Post A Comment: