Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza kufurahishwa kwake na ongezeko la ukusanyaji wa mapato katika kituo cha huduma za pamoja mpakani mwa Tanzania na Kenya cha Namanga.
Akizungumza leo Aprili 24, 2025 Namanga mkoani Arusha wakati katika ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano Dkt. Biteko ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania Kituo cha Namanga kwa kufanya kazi kwa ufanisi.
“ Nimefurahishwa sana na urahisi wa biashara na kila eneo limekuwa na ukuaji wa watu na bidhaa kwenye kusafirisha nje ya nchi ili kuleta fedha ya kigeni zitakazowezesha kufanya shughuli zingine nawapongeza sana, nawashukuru kwa kuwa na malengo makubwa ya kukusanya shilingi bilioni 124 na hadi kufikia leo mmekusanya shilingi bilioni 101 huku mkiwa na miezi kadhaa ya kuendelea kukusanya mapato” amesema Dkt. Biteko.
Amewataka watendaji hao kuendelea kuwa na utaratibu mzuri wa kurahisisha biashara kwa kuondosha mizigo inayosafirishwa kwa kutumia muda wa dakika 30 hadi 40 badala ya saa 2 kama ilivyokuwa hapo awali.
Ameendelea kusema kuwa Kituo hicho cha Namanga kilichofunguliwa mwaka 2018 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dkt. John Pombe Magufuli na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta kwa lengo la kurahisisha biashara kati ya nchi hizo mbili. Hivyo, watendaji hao waendelee kuwa mabalozi wazuri kwa kutangaza taswira njema ya Tanzania wakati wakitekeleza majukumu yao.
Awali akikagua Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Longido Samia, Dkt. Biteko amesema kuwa baada ya siku kadhaa Kampuni ya Taifa Gesi itafunga miundo mbinu ya mfumo wa gesi shuleni ikiwa ni sehemu ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Pia, Dkt. Biteko amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda kuhakikisha Shule hiyo inapata vifaa vya maabara ili wanafunzi waweze kujifunza kwa vitendo na si nadharia pekee.
“ Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya hakikisheni hizi maabara zinafanya kazi kwa kupata vifaa, tabia ya wanafunzi kuchora bunsen bunner badala ya kuziiona na kuzitumia kwa kujifunzia kwa vitendo iishe, ” amesema
Post A Comment: