Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu,Theresia Mtewele akikata utepe wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani wilaya ya Kasulu 
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu,Theresia Mtewele akiwa makini kusikiliza na kutazama matukio mbalimbali yakiendelea katika maadhimisho ya wanawake duniani 



Na Fredy Mgunda,Kasulu

 Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika Machi 8 kila mwaka Halmashashauri ya Wilaya ya Kasulu imefanya maadhimisho hayo kiwilaya katika Shule ya Sekondari Muyivozi.

Ambapo kupitia shughuli hiyo  iligawa taulo za kike,katoni za vinywaji  laini pamoja na kuendesha mijadala mbalimbali kuhusiana na namna ya kumkwamua mtoto wa kike kwa shule hiyo pamoja na wenzao wa Ntamya.  

Akizungumza katika tukio hilo Katibu Tawala wa Wilaya ya Kasulu,Theresia Mtewele ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema kuwa kwa zaidi ya miaka 30 inaposheherekewa siku hiyo kumekuwa na harakati mbalimbali za kumkomboa mwanamke zilizomsaidia kushika nafasi kubwa kwenye vyombo vikubwa vya kimaamuzi.

“Tunapoadhimisha Siku ya Wanawake mwaka 2025 tunasheherekea mafanikio ambayo wanawake tumefikia katika nyanja mbalimbali kama uwakilishi kwenye uongozi na tunaye Rais ambaye ni mwanamke tunasheherekea vitu hivi tukiwa na mifano halisi ya wanawake ambao wameweza kuingia katika nafasi kubwa za kimaamuzi,” amesema.

Naye mkimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024, Makwaya Makwaya amesema kuwa Ili mtu aweze kufikia ndoto zake ni lazima azingatie suala la nidhamu na kujituma kwakuwa haitatokea mtu kukudhamini au kukupa nafasi usipozingatia mambo hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Victoria Makyao amesema kuwa madhamisho hayo huwa na lengo la kujadili  changamoto mbalimbali zinazowakumba wanawake katika kufikia maendeleo kuona ni namna gani wanazipatia ufumbuzi.

Katika hatua nyingine Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Muyovozi,Joina Dismas amesema kuwa maadhimisho hayo yamemsaidia kujifunza wanawake ni watu kama watu wengine katika jamii hivyo wanatakiwa kuheshimiwa,kutunzwa pamoja na kuthaminiwa ili waweze kufikia ndoto zao.

Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: