Na : Jusline Marco : Arusha

Waziri wa nchi,ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Mhe.George Simbachawane amesema serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwatumia watafiti nchini katika kuibua majawabu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Akifungua Kongamano la 3 la Kimataifa kuhusu Usimamizi wa Biashara na Maendeleo ya Kiuchumi lililofanyika jijini Arusha kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Madini Mhe.Doto Biteko, Mhe.Simbachawene amewataka watafiti nchini kuendelea kuwa wabunifu ili kuweza kuleta maendeleo katika jamii na nchi kwa ujumla.

Amesema miongozo yote ya usimamizi wa mipango na mikakati ya maendeleo inalenga kukuza na kuendeleza rasilimali watu na miundombinu ,kukuza uwekezaji wa kibiashara,kulinda na kuendeleza umoja ,amani na mshikamano.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dkt.Mwigulu Nchemba,Naibu waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Exaudi Kigae amesema serikali ya awamu ya sita itaendelea kuboresha mifumo ya kisera na miundombinu wezeshi ili kupunguza gharama za uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.

Ameongeza kuwa kongamano hilo ni nyenzo mahususi ya kuwakutanisha wadau wa ndani na nje ya nchi katika utafiti na uchunguzi wa masuala ya Ubunifu ,biashara na uchumi ili kuendelea kubadilishana uzoefu, ujuzi na matokeo ya kazi za kitafiti ambao ni msingi wa maamuzi ya kisera yanayolenga kutatua changamoto za kibiashara na kiuchumi.

Ameeleza kuwa serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha mazingira wezeshi ili kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii ambapo hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya kisera ,kitaasisi na kiutawala ili kuimarisha mifumo ya utawala bora na ujenzi wa miundombinu wezeshi ikiwemo Reli ya kisasa ya SGR.

"Pamoja na mambo mengine mkutano huu umeandaliwa kwa makusudi ili kufungamanisha masuala ya tafiti na dhima ya mpango wa taifa wa tatu wa maendeleo ya taifa ya miaka mitano 2021/22 hadi mwaka 2025/26 yenye lengo la kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu."alisema Mhe.Exaud

Amesema dhima ya mpango wa tatu wa maendeleo wa taifa haiwezi kufikiwa bila kuwa na utashi ,uelewa na msimamo wa pamoja baina ya sekta ya umma na sekta binafsi kwa kutumia njia ya majadiliano ya pamoja na kufanya tafiti juu ya matokeo na takwimu za kitafiti kusudi kuwezesha watunza sera kufanya maamuzi sahihi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya wizara na taasisi ya uhasibu Tanzania Jehovanes Aikael amesema ili uwekezaji kwenye uchumi uwe endelevu, mtaji na ubora wa rasilimali watu ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kiuchumi yanatokea katika taifa ambapo dhana endelevu ya kiuchumi inahusu ukuaji wa uchumi wa muda mrefu bila kuathiri nyanja nyingine ikiwemo za kijamii mazingira pamoja na utamaduni katika nchi husika.

Amesema lengo la Kongamano hilo ni kuzungumzia ongezeko la ufanisi utakaotoa mchango katika ukuaji wa uchumi kuondoa umaskini na kuchachua maendeleo ya uchumi kwa ujumla huku mada katika mkutano huo zikijikita kwenye kuibua majawabu na namna ya kutatua changamoto zinazosababisha kutokufikia malengo mapana ya maendeleo ambayo wamejiwekea hususani katika uchumi endelevu unaohitajika.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda,Mkuu wa Wilaya ya Longido Salum Mkali amesema mkutano huo unakuja wakati ambapo sekta ya biashara katika mkoa wa Arusha imekuwa kwa kiwango kikubwa Ndani ya miaka 3 kutokana na takwimu kuonyesha kuwa Mkoa wa Arusha umekuwa ukiongezeka kwa asillimia 12 ukilinganisha na idadi ya wafanyabiashara zaidi ya 1000 kuongezeka kwa mwaka 2023.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Arusha umekuwa kitovu cha Biashara na uwekezaji kutokana na Sifa ya mkoa wenyewe kuwa lango la utalii na kitovu cha mikutano ya kimataifa hali iliyopelekea kuwa miongoni mwa mikoa inayochangia pato kubwa katika taifa na ni miongoni mwa mikoa ambayo ina kituo cha pamoja kinachokutanisha watu kutoka nchi mbalimbali.







Share To:

Post A Comment: