Balozi wa Australia nchini Tanzania, Mheshimiwa Jenny Da Rin aliwasilisha nyaraka za utambulisho wake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Australia na Tanzania zinafurahia uhusiano chanya ambao umekua ukikua kupitia uhusiano baina ya wananchi wa mataifa hayo mawili ambao ndio kiunganishi kikubwa. Australia inajivunia kuweza kutoa fursa mbalimbali za masomo kupitia mpango ya udhamini wa masomo kwa watanzania kusoma nchini Australia kupitia programu maalum ya Australia Awards Program.
Zaidi ya raia 7000 wa Australia huitembelea Tanzania kila mwaka ambapo kuna wengine ambao hujitolea kushiriki katika kuchangia shughuli za maendeleo nchini Tanzania tangu mwaka 1964.
Uwekezaji wa Australia nchini Tanzania umeendelea kukua ambapo mikataba ya madini iliyotiwa Saini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na makampuni ya Australia kwa thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 10 (sawa sawa na dola za kimarekani bilioni 3.6).
Makampuni 35 ya Australia yamewekeza kwenye utafiti wa madini, uchimbaji, uongezaji thamani na usimamizi wa maafa ya kijiolojia huku wakiweka viwango vya hali ya juu vya usimamizi, mazingira na jamii.
Mwezi Agosti mwaka huu, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano mkubwa wa madini uitwao Africa Down Under ambao ni moja ya mikutano muhimu kwa taifa la Australia kuhusiana na sekta ya madini barani Afrika, ambapo alifanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Tim Watts (Mbunge).
Kamishna wa Madini, Dkt Abdul Mwanga, hivi sasa yupo masomoni nchini Australia akichukua masomo ya madini chini ya program ya masomo ya Australia Awards program.
Australia inaunga mkono malengo ya maono ya maendeleo ya taifa ya 2025 na madhumuni ya pamoja kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa, kupitia usaidizi wa moja kwa moja katika uzalishaji kwenye kilimo, jamii, ustahimilibu wa hali ya hewa, uzalishaji wa nishati, uwezeshaji wa wanawake, afya ya uzazi na miradi ya afya kw Watoto. Tangu mwaka 2020, Australia imekuwa ikitoa dola za Australia milioni 2 kwa ajili jitihada hizi kupitia programu ya msaada wa moja kwa moja na program ya ushirikiano ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya Australia.
Balozi wa Australia nchini Tanzania, Mheshimiwa, Jenny Da Rin alisema:
“Ilikuwa ni heshima kubwa kwangu kuweza kuwasilisha nyaraka za utambulisho wangu kwa mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninamategemeo makubwa ya kuimarisha zaidi ushirikiano na serikali ya Tanzania kwa mtazamo wa kukuza zaidi ushirikiano wa kibiashara, uwekezaji na mahusiano baina ya wananchi wetu kadri muda unavyozidi kwenda.”
Post A Comment: