Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, ameitaka serikali kufanya mabadiliko ya sheria na kanuni zinazosimamia biashara ya madini ya Tanzanite, akisisitiza kuwa zuio la kuuza madini hayo nje ya eneo la Mererani linachangia hasara kubwa kwa taifa.
BONYEZA HAPA KUMSIKILIZA ZAIDI MBUNGE MRISHO GAMBO
Gambo ameyasema hayo Ijumaa, Oktoba 18, 2024, wakati wa mkutano na wafanyabiashara wa madini na ma-brokers uliofanyika katika Soko la Madini, mkoani Arusha.
Akizungumza kuhusu namna ambavyo sera za sasa zinaathiri sekta ya madini, Gambo amefafanua kuwa katika miaka ya nyuma, thamani ya madini ya Tanzanite ilikuwa juu, ikifikia hadi dola 2000 kwa gramu, lakini kutokana na maamuzi yasiyo sahihi na ubinafsi, thamani hiyo imekuwa ikishuka siku baada ya siku.
"Taifa linapata hasara, nchi inapata hasara kwa sababu ya ubinafsi. Unailinda Mererani, unaliua taifa," amesema.
Gambo pia ameeleza kwamba licha ya kuwa Mererani ndiyo eneo pekee la kuchimba Tanzanite, serikali haipaswi kuzuia madini hayo kuuzwa sehemu zingine ndani ya nchi. Alilalamika kuwa kwa sasa ni rahisi kupeleka madini hayo nje ya nchi, kama vile India na Marekani kuliko kuyapeleka katika miji ya Tanzania kama Arusha au Dar es Salaam.
"Leo ukienda Mererani na ukinunua madini yako, ukilipa mrabaha, unaruhusiwa kuyapeleka India, Marekani, Dubai, Kenya, lakini huruhusiwi kuleta Arusha au Dar es Salaam," amesisitiza Gambo. Leo Arusha inajivunia kuuza mchanga na kokoto, na siyo madini ya Tanzanite tena. Hiyo si habari njema. Mapato yameshuka, na ukienda kwenye utafiti uliofanywa na Wizara ya Madini yenyewe, moja ya sababu ya kushuka kwa madini ni zuio la kutaka madini yawe Mererani peke yake," amesema Gambo.
Post A Comment: