Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Msalala Ndg. Rose Robert Manumba amezungumza na kutoa maelezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Wadau mbalimbali wakiwemo Wakuu wa idara , Watendaji wa vijiji na Kata , viongozi wa dini na viongozi wa Vyama vya Kisiasa. Amewataka Viongozi hao kushiriki kwa pamoja katika utoaji wa elimu kwa jamii inayowazunguka ili kujenga uelewa na kurahisisha wananchi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika 27 Novemba 2024.


Aidha, Mkurugenzi huyo aliwaeleza Wadau hao kuwa maelezo hayo yametolewa siku sitini na mbili kabla ya siku ya uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha kuwa taratibu zote zinafuatwa na kwamba wapiga kura pamoja na wagombea wanapata taarifa zote zinazohitajika kwa wakati.

Bi Rose Robert Manumba alieleza kuwa maelekezo haya yanafafanua hatua zitakazoongoza mchakato wa uchaguzi, kuanzia uandikishaji wa wapiga kura, uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea, uteuzi wa wagombea na tarehe ya siku ya uchaguzi. Maelekezo haya yanalenga kutoa mwongozo ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na usawa na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Kwa upande wa Viongozi wa dini wameshukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia uhuru wa kuabudu na siku ya uchaguzi kupangwa kufanyika siku ya kazi pasipo kuathiri siku za kuabudu.







Share To:

Post A Comment: