Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 5 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ili kusaidia kugharamia upatikanaji na utoaji wa huduma matibabu ya Ubingwa na Ubingwa Bobezi kwa wananchi wenye uhitaji kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Julai 19, 2024 alipotembelea Hospitali ya Taifa MUHIMBILI kwa lengo la kuangalia huduma zinazotolewa za kibingwa na ubobezi kupitia fedha zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kuhakikisha wananchi wasiokuwa na uwezo wakumudu gharama kubwa za matibabu ya Ubingwa na Ubingwa bobezi na wenye uhitaji wanapata huduma hizo." Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema kiasi cha Shilingi Bilioni 2.6 zimetolewa kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo awamu ya kwanza zimegharamia wagonjwa wa kupandikiza Figo ( wagonjwa 6); kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia kwa watoto 10, kupandikiza ULOTO wagonjwa 5 pamoja na kusaidia watoto 10 wenye matatizo ya mfumo wa Ulolojia.

Kwa upande wao, wanufaika wa huduma hizo, kwa pamoja wameiomba Serikali kushusha huduma hizo za Ubingwa Bobezi ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa ambapo kuna wananchi wengi anbao pia wanahitaji huduma hizo.

Waziri Ummy ameahidi kulifanyia kazi jambo hilo kwa kuona ni hatua gani za awali za Ubingwa Bobezi zinaweza kuanza kutolewa katika ngazi hizo ili kila Mtanzania aweze kunufaika na huduma hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili amemuhakikishia Waziri wa Afya kuwa Hospitali hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi na kutekeleza Sera, Miongozo na Maelekezo ya Serikali katika kuwahudumia wananchi wanaopata huduma katika vituo Viwili vya Upanga na Mloganzila.




Share To:

Post A Comment: