Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amewasihi Mafundi Sanifu kuzingatia miongozo ya taaluma zao na kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu ili kuwezesha Taifa kupata thamani ya fedha za miradi inayotekelezwa.
Kasekenya amezungumza hayo Mei 24, 2024 jijini Dodoma wakati akifunga Mkutano wa Sita wa Mafundi Sanifu wa Mwaka 2024 na kusisitiza kuwa Taifa linawategemea Mafundi Sanifu hao katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kihandisi katika Sekta ya Ujenzi.
"Niwasihi Mafundi Sanifu kuhakikisha tunaona thamani ya fedha katika ujenzi wa miradi mnayotekeleza kwa kufanya kazi kwa uadilifu na ubora hii itaweza kusaidia nchi kuokoa fedha, kwani Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kiu yake ni kuleta maendeleo na mageuzi kwa miradi inayotekelezwa", amesema Kasekenya.
Aidha, Kasekenya ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Bodi ya ERB na kuhakikisha kwamba maazimio yaliyofikiwa katika mkutano huu yanafanyiwa kazi na matokeo yake yanachangia katika kukuza uchumi wa nchi na katika kufikia malengo ya Maendeleo Endelevu ya nchi yetu.
Kadhalika, Kasekenya amewasisitiza Mafundi Sanifu kufanyia kazi maazimio waliojiwekea katika mkutano huo ili kupata matokeo chanya ambayo Serikali wanayatarajia kupitia kada hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Wakili Menye Manga, amesema kuwa Mkutano huu umelenga kubadilishana uzoefu kupitia teknolojia mbalimbali zinazoibuka duniani kama matumizi ya akili mnemba katika Sekta mbalimbali ili kuweza kusambaza utaalam huo nchini.
Post A Comment: