Na John I. Bera - Arusha


Timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya Mpira wa Miguu, leo  Aprili 18, 2024 imefuzu hatua ya makundi kwenye Mashindano ya Mei Mosi yanayofanyika Jijini Arusha.


Akizungumza mara baada ya kufuzu kwa kuifunga Timu ya Chuo cha Ufundi cha Arusha  (ATC) kwa goli mbili kwa nunge, Kapteni wa Timu hiyo, Bw. Arnold Elias amesema ushindi huo umetokana na juhudi mbalimbali za Wachezaji, Viongozi pamoja na Waalimu ambao wamekuwa wakipambana kuhakikisha kuwa Wizara inapata ushindi


Ameongeza kuwa, ushindi huo utaleta chachu na ari zaidi kwani kwa kufanya hivyo, kuitangaza Wizara pamoja na majukumu yake ikiwemo kuutangaza utalii wa ndani.

"Tunaushukuru Uongozi wa Wizara ya Maliasili kwa ujumla, umetupa hamasa kubwa tunawahakikishia viongozi kuwa tutapambana ili kufikia malengo na kufika fainali kwani tunaposhinda tunatangaza utalii" Amesema Elias


Kwa upande wa Kocha wa Timu hiyo, Bw. Abdallah Juma amewapongeza wachezaji kwa jitihada zao za kuhakikisha wanaipambania Wizara huku akisisitiza ya kuwa wao kama Timu watahakikisha wanailetea Wizara Ushindi


" Nawapongeza Wachezaji kwa ujumla, wamepambana sana kuhakikisha wanailetea Wizara ushindi na tumeweza kufuzu hatua inayofuata" Amesema Juma


Naye mfungaji bora kwa upande wa Wizara, Bw. Newton Mlai amesema ataendelea kujituma kwa ari kubwa ili kuhakikisha wanafuzu kwenye hatua inayofuata ili kutwaa ushindi.



 Aidha, Bw. Mlai ameshukuru wachezaji wenzake wote kwa kujituma na kupambana pia ameupongeza uongozi Mzima wa Wizara kwa uongozi mahiri unaosababisha matokeo ya ushindi.


Katika Kundi Wizara ya Maliasili imefuzu pamoja na Timu kutoka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) huku Timu zingine za TPDC pamoja na Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC) zikishindwa Kufuzu kwa hatua inayofuata.


Sanjari na Kufuzu huko, Michezo mbalimbali imechezwa leo ikiwemo Mchezo wa Kamba kwa upande wa Wanaume na Wanawake ambapo Wizara imeibuka Mshindi kwa point 2 kwa sifuri dhidi ya RUWASA kwa upande wa Wanaume na Point 2 kwa Sifuri dhidi ya Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO)



Share To:

ASHRACK

Post A Comment: