1000000726


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Rukwa kumsimamia Mkandarasi Kampuni ya China Geo-Engineering Corporation anayejenga barabara ya Matai – Kasesya; sehemu ya kwanza Matai – Tatanda (km 25) kwa kiwango cha lami ili uweze kukamilika ifikapo mwezi Novemba, 2024.

Bashungwa ametoa agizo hilo Aprili 09, 2024 mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambao umefikia asilimia 37.6 na kusisitiza kufuatwa kwa viwango vya ubora kama ilivyo katika mkataba pamoja na kupata thamani ya fedha katika mradi.

“Niagize TANROADS muendelee kusimamia yale yaliyopo kwenye mkataba katika mradi huu na kwa upande wa Serikali baada ya ziara hii nitahakikisha Mkandarasi analipwa madeni yake ili kasi ya ujenzi iweze kuongezeka”, amesisitiza Bashungwa.

1000000725

Bashungwa amemtaka Mkandarasi huyo kujenga barabara hiyo kwa viwango kulingana na mkataba maana ubora wa kazi hiyo ndio utampatia fursa ya kupewa miradi mingine ya kutekeleza.

Bashungwa ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua Mkoa wa Rukwa kama moja ya Mkoa wa Kimkakati wa kukuza uchumi wa Nchi kwa kuunganisha miundombinu ya barabara ili tuwezesha Wananchi kufanya biashara pamoja na nchi jirani za Zambia na DRC Kongo.

Aidha, Bashungwa ameeleza kutokana na umuhimu wa barabara hiyo kiuchumi ataomba kibali kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili Mkandarasi huyo huyo aweze kuendelea kilometa 25 zilizobakia hadi kufika Kisesya mpakani mwa Tanzania na Zambia.

Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa Eng. Mgeni Mwanga amesema ujenzi wa barabara ya Matai – Tatanda (km 25) unahusisha ujenzi wa madaraja matatu ambapo Daraja la Kanyele limekamilika asilimia 99, Daraja la Mpala limekamilika asilimia 98 na Daraja la Matai limekamilika asilimia 74.
IMG-20240409-WA0129
IMG-20240409-WA0119
IMG-20240409-WA0115
IMG-20240409-WA0125
IMG-20240409-WA0123
Share To:

Post A Comment: