Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Paul Christian Makonda leo Aprili 18,2024 amekagua maandalizi na marekebisho ya uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid Mjini Arusha, Uwanja uliopangwa kufanyika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yanayotarajiwa kufanyika Mei Mosi mwaka huu 2024.

Mgeni wa Heshima katika maadhimisho hayo kulingana na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mh. Paul Christian Makonda anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Tumaini Nyamhokya Rais wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi nchini Tanzania pamoja na Makamu mwenyekiti wake na wakuu wengine wa idara mbalimbali waliambatana na Mheshimiwa Mkuu wa mkoa Paul Makonda kwenye ukaguzi huo wa maandalizi ya sherehe hizo kubwa kwa wafanyakazi wa sekta mbalimbali.

Nyamhokya ameviambia vyombo vya habari kuwa maandalizi yanaendelea vyema na kila kamati inafanya kazi yake kikamilifu ili kuhakikisha kuwa sherehe hizo zinakuwa nzuri na za kuvutia.

Nyamhokya amesema kufanyika kwa shughuli hiyo mkoani Arusha ni fursa pia kwa wakazi wa Arusha na wageni mbalimbali kwani watapata fursa za kuuza bidhaa mbalimbali za vyakula, vinywaji na sehemu za kulala wageni watakaohudhuria maadhimisho hayo kwa mwaka huu ambapo tayari baadhi ya wageni wamekwishaanza kuwasili mkoani hapa.

Mei Mosi ama siku ya Wafanyakazi duniani ni siku ya mshikamano kwa Wafanyakazi mbalimbali katika kusimamia na kuunga mkono Haki, Wajibu na Dhamana ya wafanyakazi kote ulimwenguni katika mchakato wa kufikia maendeleo endelevu.

Kwa mara ya pili tangu kuteuliwa kwake, Mheshimiwa Mkuu wa mkoa wa Arusha Mh.Paul Makonda atampokea mkoani kwake Mh.Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakuu wa serikali, mara ya kwanza ikiwa ni wakati wa Misa maalum ya kumbukumbu ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Hayati Edward Moringe Sokoine.


Share To:

Post A Comment: