Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Arusha Thomas Loy Sabaya amempa mwezi mmoja Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Steven Ulaya kukamilisha ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Kamwanga.
Ole Sabaya ametoa maagizo hayo katika ziara yake na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya mkoa wa Arusha ya kukagua Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika wilaya hiyo ikiwemo shule ya Sekondari Kamwanga itakayogharimu kiasi cha Shilingi milioni 528.28 kutoka mradi wa kuboresha elimu ya Sekondari Tanzania (SEQUIP).
Kamati hiyo ya siasa imeonyesha kuchukizwa na kutoridhishwa na kusuasua kwa ujenzi wa shule hiyo ambayo ilitakiwa kukamilika tangu mwaka jana ambapo mpaka sasa wanafunzi wanaendelea kutembea umbali zaidi ya kilomita 30 kwenda kwenye shule zilizopo katika Kata za jirani.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido Steven Ulaya ameieleza kamati ya siasa kuwa kukosekana kwa eneo la ujenzi wa shule hiyo na kulazimika kutafuta eneo lingine na kuahidi kamati hiy kuwa ataendelea kusimamia kwa karibu na kuhakikisha hadi kufikia tarehe 29 Machi mradi huo utakuwa umekamilika.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Enduimet Mwl. Hassan Hassan, amesema kuwa, mradi huo unatekelezwa kwa kiasi cha shilingi milioni 584.2, fedha kutoka Serikali Kuu kupitia mpango wa kuboresha Elimu ya Sekondari Tanzania (SEQUIP).
Amesema kuwa, Mradi huo unajumuisha ujenzi wa jengo la Utawala, vyumba 8 vya madarasa, maabara tatu za somo la Fizikia, Kemia na Baiolojia, Maktaba, jengo la TEHAMA,pamoja na matundu 20 ya vyoo.
Aidha mradi huo ukikamilika unatarajiwa kuboresha mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kupunguza msongamano katika shule zingine za Sekondari.
Post A Comment: