ATAKA MRADI HUO KUKAMILIA KABLA YA TAREHE 30 JUNI, 2024

NAIBU Waziri wa Maji  Mhandisi Maryprisca Mahundi  amemtaka Meneja  wa RUWASA Mkoa wa Njombe Mhandisi. Sadick Chakka, kuhakikisha  anasimamia wananchi ambao wapo jirani na chanzo cha maji cha Igongwi  kilichopo Mkoani humo,  wawe  wa kwanza kupata huduma ya maji kabla haijafika maeneo mengine yaliyopangwa.

Kadhalika ametoa maagizo kwamba mradi huo ukamilike kabla ya tarehe 30 Juni, 2024 ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Mahundi ameyasema hayo leo Machi 15,  2024,akiwa Mkoani Njombe kwenye muendelezo wa ziara na Kamati ya Kudumu  ya Bunge ya Maji na Mazingira ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji. 

"Utekelezaji wa kipande hiki kwa sehemu kubwa umekamilika lakini hakijaanza kutoa huduma kutokana na wananchi wa Kijiji cha Luvuyo kuzuia maji kwenda kwenye vijiji vya Kitulila, Madobole, Luponde na Njoomlole,

"Wananchi hawa wamezuia ukamilishaji wa kipande hiki hadi hapo ujenzi wa mradi kwenye Kijiji chao utakapo kamiliaka hivyo fanyeni mhakikishe wao wanakuwa wa kwanza kupata huduma kabla hamjapeleka maeneo mengine" amesema Mhandisi Mahundi 

Amesema Mradi huo unatekelezwa katika vipande ambapo kukamilika kwake kunatarajia kunufaisha wananchi wapatao 10,034.

Kwa upande wake Mwenyekiti  wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe.Jackson Kiswaga  ameipongeza Wizara ya Maji kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi maji

Ikumbukwe kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.15. Kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 71 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024.


Share To:

Post A Comment: